Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonyesha dhamira ya serikali yake katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mafuru, Wilayani Mvomero.
Hayo yamebainishwa Januari 17 mwaka huu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mafuru alipotembelea kukagua jengo la zahanati ambalo limefikia hatua ya lenta ikiwa ni nguvu za wananchi.
Mwl. Linno amewapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa na wazo la kujenga zahanati huku akibainisha kuwa fedha zilizotolewa na Serikali ni kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi hao zitatumika kwa ujenzi wa miundombinu iliyosalia na kuhakikisha zahanati hiyo inaanza kutoa huduma haraka iwezekanavyo.
"...niwapongeze kwanza kwa kuwa na wazo la kuwa na zahanati na mkaanza boma...Serikali tukufu inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta mzigo hapa, milioni 50 ili kukamilisha zahanati ianze..." amesema Mwl. Linno.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewataka wananchi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba Zahanati ijengwe kwenye kiwango kinachohitajika ili kuhakikisha kuwa zahanati inaanza kutoa huduma kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
Sambamba na hilo, Mwl. Linno ameuagiza uongozi wa kijiji hicho kuhakikisha inaunda kamati ya ujenzi itakayokuwa imara ili mradi ukamilike kwa wakati na sio kwenda kutumia fedha hizo vibaya.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amewataka wananchi kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira ikiwemo matumizi sahihi ya vyoo huku akiwataka kutumia maji yaliyochemshwa ili kujikinga na magonjwa ya kuhara na kutapika.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Philipina Philipo amesema Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo imetoa shilingi milioni 50 ambazo tayari zimeingizwa kwenye akaunti ya kijiji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo itasaidia kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya maeneo mengine.
Pamoja hayo, Dkt. Philipina amewakumbusha wananchi kuendelea kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira kama kunawa mikono kwa maji safi, kuchemsha maji kabla ya kuyatumia hususan kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha ili kujikinga na magonjwa ya kuhara.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafuru ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati hiyo, pia amesema Kijijini hapo mifugo bado inasumbua kwenye mashamba ya wakulima na kupelekea wananchi kushindwa kujitoa kwenye kazi ya ujenzi kwa sababu wanatumia muda mwingi kulinda mashamba yao.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.