Taasisi isiyo ya kiserikali ya PAMS Foundation imepongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa maeneo ya vijijini kwa kuwapatia mitungi ya gesi bila gharama yoyote, hatua inayosaidia kuhifadhi mazingira na kuboresha afya za watumiaji.
Pongezi hizo zimetolewa Julai 19, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa wakati akizungumza na wananchi wa kijiji Cha Digoma na Maskati kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa misitu unaotekelezwa na Taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Tawala huyo amesema juhudi za PAMS Foundation zinachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa matumizi ya kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha nishati, hatua inayosaidia pia kupunguza uharibifu wa misitu.
“...tena niwasifu sana na ukweli mmekuwa mkishirikiana sana Serikali hasa kile kitendo mnachofanya cha kuwapa hawa wananchi gesi ili tupunguza ya kuni...huu mpango naomba uendelee...amesema Katibu Tawala.
Aidha, ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinala barani Afrika katika kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia nishati safi na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa huku akiongeza kuwa nchi inamalengo ya kufikia asilimia 80 mwaka 2030 wananchi wawe wanatumia nishati safi.
Sambamba na hilo, Dkt. Mussa amesema Mkoa wa Morogoro utaendelea kutafuta wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya lengo inafikiwa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Ndg. Paulo Faty amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa kukagua utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa misitu katika Wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka PAMS Foundation, amesema kuwa ugawaji wa mitungi hiyo ya gesi ni sehemu ya kutoa hamasa kwa wananchi ambao wamejiunga katika mradi huo. Aidha, amebainisha kuwa katika kijiji cha Maskati wamepata eneo la kutekeleza miradi huo lenye ekari 250 ambapo zoezi la upimaji linaendelea.
Nao baadhi ya Wananchi wa Vijiji hivyo wameonesha kufurahishwa kwao na uwepo wa mradi huo ambao utawasaidia kurudisha uoto wa asili na kuwawezesha kupata kipato
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.