Wizara ya Maliasili na Utalii imezielekeza Taasisi zake za TANAPA na TAWA kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero katika kutatua changamoto ya tembo ambao wamekuwa wakisababisha madhara kwa wananchi ikiwemo vifo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula (Mb) wakati akizungumza mbele ya mamia ya wakazi wa Vijiji vya Mangae, Doma na Mkata Wilayani Mvomero wakati wa Operesheni ya kurudisha makundi ya Tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Naibu Waziri amesema kwa kutumia helikopta makundi ya tembo 45 yaliyokuwa kwenye makazi ya wananchi yamerejesha hifadhini katika zoezi linalomalizika leo.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa zoezi la kuondoa tembo kwenye makazi ya wananchi kwa kutumia helikopta litaenda sambamba na ufungaji wa mikanda yenye mawasiliano ili kurahisisha ufuatiliaji wa mienendo ya makundi ya tembo kwenye maeneo ya Mvomero na kuwapa Askari wa Uhifadhi taarifa kwa haraka pale ambapo watakuwa wametoka kwenye maeneo yao.
Pamoja na zoezi la kuondoa tembo, Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa vifaa vya kufukuzia tembo vikiwemo tochi kubwa zenye mwanga mkali, pilipili, fataki na honi zenye mlio mkali.
Naibu Waziri pia alieleza jitihada zilizofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuthibiti wanyama waharibifu, ikiwemo utoaji wa mafunzo ya matumizi ya teknolojia rahisi ili kahikikisha kuwa changamoto ya wanyama waharibifu aina ya tembo inadhibitiwa na wananchi.
Aidha Mhe. Kitandula alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miongozo na uwezeshaji wa kifedha hivyo kufanikisha suala hilo katika kipindi chake cha miaka mitatu ili kuwahakikishia usalama wananchi na uhifadhi endelevu nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuwezesha zoezi la kufukuza tembo kwa kutumia Helikopta kwani changamoto ya tembo imekuwa ni kero ya muda mrefu wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland amesema uwezeshaji wa zoezi hili ni faraja kwa wananchi kwani tembo wamekuwa wakileta uharibifu mkubwa wa mali na kuhatarisha usalama wa wananchi hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia kuepukana na changamoto hiyo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.