Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) wametangaza rasmi kuanza kununua mazao kupitia vituo vyake vilivyopo katika maeneo mbalimbali Tanzania nzima, fursa ambayo Wanamvomero kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiililia.
Akiongea mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Bungoma, Kata ya Mkindo Wilayani Mvomero, Mwakilishi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula,NFRA kanda ya kipawa Ndg. Mgeni Mussa amesema kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiwafikia wakulima wa nafaka maeneo mbalimbali nchini na sasa neema hii imewafikia wakulima wa Mvomero.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akizindua mwongozo wa ununuzi wa mazao ya wakulima kwa wafanyabiashara, amewataka wafanyabiashara wazingatie mpango huo ili Serikali na Halmashauri ziweze kukusanya ushuru ili Serikali itoe huduma za msingi kwa wananchi wake.
“Tunaomba wanunuzi wa mazao wapitie Halmashauri wapewe vibali vya ununuzi wa mazao. Serikali ya awamu ya sita ina nia ya kulinda maslahi ya wakulima.Tuzalishe mazao ya kutosha, shule nyingi za Mvomero pia zinahitaji chakula.” Amesema Mkuu wa Wilaya hiyo wakati akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Bungoma.
Kuhusu fursa iliyoletwa na Wakala wa hifadhi ya Chakula (NFRA) Mkuu wa Wilaya amewaasa wakulima wa Mvomero kuitumia fursa hiyo vizuri kwani bei ya ununuzi inayotolewa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ni bora kuliko ile inayotolewa na wafanyabiashara walanguzi wasiozingatia maslahi ya Wakulima.
“Zali limetuangukia Wanamvomero, naomba tutumie fursa hii na pia tulinde amani yetu. Wanunuzi wamekuja hapa kwa kuwa kuna amani.” Aliongeza Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Kipawa Ndg. Mgeni Mussa amewahakikishia wakulima uhakika wa malipo yao mara tu baada ya mauzo. “Malipo ni ndani ya masaa 24. Kama ukikamilisha kila kitu, mara baada tu ya mauzo, pesa yako unaipata kesho yake.”
Kata ya Mkindo ni moja ya Kata zinazozalisha mpunga kwa wingi sana kwa Mkoa wa Morogoro. Serikali ya awamu ya sita imewekeza Bilioni 5.6 kuanzia Septemba mwaka 2022 kwa mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgongola ambayo itawahakikishia wakulima uhakika wa kulima mazao mwaka mzima.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.