Chuo Kikuu cha Mzumbe kimeonyesha mshikamano na Serikali katika kukuza upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa kukabidhi vitabu 400 vya sheria kwa ajili ya kuunga mkono Kampeni ya Mama Samia Legal Aid Wilayani Mvomero.
Makabidhiano hayo yamefanyika Julai 21, 2025 katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambapo kitabu hicho kinaitwa Utekelezaji wa Sheria, kitatumika kutoa msaada wa kisheria kwa viongozi wa Serikali za Vijiji katika Wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Paulo Faty ameushukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuona umuhimu wa kutoa msaada wa kisheria kwa viongozi wa ngazi ya chini ambao muda mwingi wanakaa na wananchi na hata maamuzi ya kisheria uanzia kwao.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo amebainisha kuwa utoaji wa vitabu hivyo ni sehemu ya kuunga mkono Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid) ambapo Viongozi pamoja na wananchi watanufaika na uwepo wa vitabu hivyo.
Kwa upande wake, Afisa Maktaba kutoka Chuo Mzumbe Bi. Sarah Mwambalasa amesema wanakabidhi vitabu 400 vya utekelezaji wa sheria ambavyo vina thamani ya shilingi 4,000,000 vinatarajiwa kuwasaidia wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na wajumbe wa Serikali ya Vijiji.
Naye, Mhadhiri Msaidi Kitivo cha Sheria Bw. Hamisi Yange kutoka Chuo hicho amesema vitabu hivyo vimeandikwa na waandishi wawili, pia vinatoa muongozo wa kutambua na kufahamu Sheria mbalimbali zilizopo hapa nchini huku akibainisha kuwa kina sura 16.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.