Katika tukio la kushtua wakazi wa kijiji cha Lukenge wilayani Mvomero, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Anselem John, anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 60 amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mamba wakati akinawa maji kwenye mto Mkindo uliopo kando na shamba lake.
Kwa mujibu wa taarifa za mashuhuda, wamesema tukio hilo limetokea januari 21, mwaka huu ambapo marehemu alikuwa akinawa maji baada ya kukamilisha shughuli zake za kilimo ndipo huo aliposhambuliwa na mamba na kupelekea kifo chake. Mwili wa marehemu ulipatikana alfajiri ya Januari 22, 2025 kwenye kingo za mto huo ukiwa na majeraha makubwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli, amefika katika eneo la tukio na kutoa pole kwa familia ya marehemu na wakazi wa kijiji hicho. Akizungumza na wanakijiji, Mhe. Nguli ametoa agizo kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kushughulikia mamba walioko kwenye mto huo haraka iwezekanavyo.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kupitia taarifa ya wanakijiji zaidi ya watu 17 wamepoteza maisha kutokana na mamba lakini wananchi hawakuwahi kuripoti sehemu yoyote hivyo, ameitaka TAWA kuhakikisha wanadhibiti mamba hao ili kuepusha kutokea kwa vifo zaidi vinavyotokana na mashambulizi ya mamba.
Mhe. Nguli amebainisha jitihada ambazo Serikali itachukua kwa haraka ikiwemo kurekebisha pampu ya kisima cha maji katika kijiji hicho ili wananchi waache kwenda mtoni na badala yake watumie maji ya kisima hiko.
Naye, Afisa wa wanyamapori kutoka TAWA Bw. Paul Mbeya amesema kuwa taasisi hiyo inaendesha zoezi la uvunaji wa mamba ambalo lilianza tangu mwaka 2024, huku akiongeza kuwa kupitia agizo la Mkuu wa Wilaya wanaanza zoezi la kusaka mamba hatarishi katika mto huo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kufanikisha jambo hilo.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.