Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, leo Machi 2, 2025 ametembelea vituo mbalimbali vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Mzumbe, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na kushuhudia wananchi wengi wakiwa wamejitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.
Aidha, Mhe. Jaji Mwambegele amewataka wananchi ambao tayari wamejiandikisha na kuboresha taarifa zao kuwahamasisha wananchi wengine kujitokeza kuboresha taarifa zao kabla zoezi hilo kuhitimishwa tarehe 7 Machi, 2025.
Mwenyekiti huyo wa Tume ameambatana na Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha, Afisa Muandikishaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Jimbo la Mvomero Bi. Mary Kayowa pamoja na Waratibu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Vituo vilivyotembelewa na Mwenyekiti huyo wa Tume huru ya Uchaguzi ni pamoja na Kituo Cha Vikenge, Shule ya Msingi Masanze, Kituo cha Stendi ofisi ya Mtendaji wa Kijiji pamoja na Kituo cha Mailikumi vituo vyote vipo Kata ya Mzumbe.
Zoezi hilo la uboreshaji limeanza tangu Machi Mosi, 2025 na litaendelea hadi Machi 7 mwaka huu likiwa na kaulimbiu isemayo "Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi".
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.