Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imezindua rasmi zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa Halmashauri hiyo kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakao fanyika Novemba 27, 2024. Elimu hiyo inalenga kuwapa uelewa wananchi kuhusu mambo muhimu ya uchaguzi huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Septemba 16, 2024 Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Mwl. Linno Mwageni amesema uchaguzi huo utahusisha Vijiji 180, Vitongoji 687 ambapo wananchi watachagua Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji pamoja na wajumbe wao huku akibainisha kuwa maandalizi ni mazuri.
Aidha, Mwl. Mwageni amesema Halmashauri hiyo imejiandaa vizuri ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki yake ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi huo na kueleza kuwa zoezi la kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura litaanza rasmi Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu.
Sambamaba na hilo, Mkurugenzi huyo ametaja vigezo vitakavyo zingatiwa wakati wa kujiandikisha vikiwemo anayejiandikisha awe ni raia wa Tanzania, awe na umri usio pungua miaka 18, awe ni mkazi wa Kijiji au Kitongoji husika na pia awe na akili timamu.
Katika hatua nyingine, Mwl. Mwageni amesema katika zoezi hilo la utoaji elimu litashirikisha wadau na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini, Mila pamoja na Wazee Maarufu lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu kuhusu uchaguzi huo.
Kaulimbiu ya uuchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 inasema “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki uchaguzi”
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.