Wilaya ya Mvomero imeazimia kuwasilisha andiko maalum serikalini ili kuomba kuongezewa bajeti kwa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo.
Azimio hilo limefikiwa leo Februari 18, 2025 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilicholenga kupitia na kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Aidha, wajumbe wa kikao hicho wamejadili changamoto kubwa ya ubovu wa barabara zinazosimamiwa na TARURA, hali inayosababisha usumbufu kwa wakazi na wafanyabiashara katika shughuli zao za kila siku.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amesema hali ya uzalishaji katika Wilaya hiyo ni mkubwa lakini miundombinu ya barabara sio rafiki, hata hivyo amesema kuwa kuna wakati TARURA inashindwa kutekeleza miradi yake kutokana na bajeti kuwa ndogo, hivyo kuna haja kama Wilaya kuisaidia TARURA ili iongezewe bajeti.
"...ili tuwasaidie lazima tutoke na maazimio ya hali halisi ya barabara zetu hapa ili tupeleke juu kwa ajili ya msaada waongezewe bajeti..." amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Judith Nguli ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kuandaa mpango wa bajeti ambayo itaenda kuivusha Halmashauri hiyo, huku akimshauri Afisa Mipango wa Halmashauri kuongeza vyanzo vingine vya mapato vikiwemo ushuru wa viwanja, Vibali vya ujenzi pamoja na hoteli, nyumba za wageni, vituo vya mafuta na mashine za mbao.
Akiwasilisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Amos Kanige amesema kuwa Halmashauri inakisia kukusanya jumla ya shilingi Bilioni 59,976 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri, Ruzuku ya Serikali kuu na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Mvomero Mhandisi Said amesema kuwa mpango wa bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 TARURA inatajaria kutumia shilingi Bilioni 3,943.762 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.