Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli leo Agosti 15, 2024 ameongoza kikao cha wadau wa Sekta za Kilimo na mifugo kwa lengo la kuhamasisha urasimishaji wa Ardhi kwa wakulima na wafugaji kuelekea utekelezaji wa Kampeni ya Tutunzane Mvomero 2023 – 2028 ambayo ilizinduliwa Agosti 3, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Nguli amesema zoezi lililopo kwa sasa ni kuhamasisha wakulima na wafugaji kurasimisha ardhi zao ili waweze kupatiwa hati miliki za mashamba hayo na hatimae wapatiwe mbegu za malisho na ufuta kwa ajili ya kupanda.
“…leo nina mkutano huu wa kuhamasisha urasimishaji wa ardhi kwa wakulima na wafugaji, mwenye eneo akamilikishwe kihalali, apate hati yake, apate malisho yake, achimbe kisima chake ili aweze kuondokana na haya maugomvi ambayo yanatuharibia Amani ya nchi yetu…” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, amesema kwa niaba ya Serikali atawasaidia wakulima na wafugaji kumili ardhi huku akibainisha kuwa Serikali itatoa wataalam wa kilimo na mifugo ili waweze kuwahudumia kwa karibu kipindi chote cha kilimo cha malisho na ufuta.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wakulima na wafugaji kutumia fursa ya uwepo kampeni ya TUTUNZANE MVOMERO kupima maeneo yao kwa kuwa zoezi hilo hutumia gharama ndogo ukilinganisha na upimaji wa ardhi nje ya kampeni hiyo.
Naye, Afisa Mifugo Mwandamizi Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Onesmo Ngenzi amesema lengo la Kampeni hiyo ni kuwamilikisha Ardhi wafugaji hivyo hawana budi kununua ardhi ya kutosha, ameongeza kuwa Wizara itahakikisha wafugaji na wakulima wanapata mbegu ili waweze kuzipanda katika mashamba yao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro Bw. Julius Mwakafwila amebainisha kuwa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi kuna aina Tatu za Ardhi ambazo ni Ardhi ya Kijiji, Ardhi ya Jumla (kawaida) na Ardhi ya Hifadhi. Pia amesema wakati wa zoezi la upimaji wa ardhi kutakuwa na uzingatiaji wa aina za ardhi zilizobainishwa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.