Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Wilaya ya Mvomero imefanikiwa kuondosha dawa zilizoingizwa nchini kinyume na taratibu katika operesheni maalum ya kudhibiti usambazaji wa dawa haramu na zisizo salama kwa matumizi ya binadamu.
Operesheni hiyo, iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ilibaini uwepo wa dawa ambazo ziliingizwa bila kufuata sheria na bila kibali cha TMDA zilitolewa na mfadhili kwa ajili ya zahanati katika kijiji cha Mela, Kata ya Mangae, hali inayohatarisha afya za wananchi.
Akizungumza Februari 15, 2025 kwenye mkutano na wananchi wa kijiji cha Mela Afisa wa TMDA Bi. Riziki Shemula ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa ya uwepo wa dawa hizo amefanya ugakuzi ambapo imebainika kuwa dawa hizo hazitambuliki na Serikali kwakua hazijasajiliwa na mamlaka husika, mfadhili huyo hakuwa na kibali cha kuingiza dawa nchini.
Aidha, ukaguzi huo pia umebaini kuwa uhifadhi wa dawa hizo haukufuata taratibu maalum za kuhifadhi dawa, pia dawa hizo muda wake wa matumizi umeisha.
Kufuatia maelezo ya Afisa wa TMDA, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ametoa maelekezo kwa niaba ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya akiwataka wafadhili wanaojitolea kuleta misaada kwa wananchi wa Wilaya hiyo wafuate sheria, taratibu na miongozo ya nchi. Aidha, ameongeza kuwa dawa hizo zinatakiwa kuteketezwa kwakua si salama tena.
Sambamba na hilo, Mhe. Judith Nguli amemuagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa zahanati hiyo inaanza kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mangae Mhe. Christopher Maarifa amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa maelekezo aliyoyatoa na kuhaidi kuyafanyia kazi.
Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kwamba inajali Afya za wananchi wake.
Dawa hizo zina uzito wa kilo 150 na zinathamani ya shilingi 43, 126, 517/=
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.