Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Ndg. Godfrey Eliakimu Mzava amemtaka mmiliki wa kituo cha mafuta cha Matemba kilichopo katika kijiji cha Mziha Wilayani Mvomero kuwasilisha kwa kiongozi huyo taarifa za mikataba ya wafanyakazi wa kituo hicho
Ndg. Godfrey Mzava ametoa agizo hilo Aprili 20 mwaka huu wakati akizindua mradi wa kituo cha Mafuta kilichopo Kijiji cha Mziha Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 amesema kuwa wafanyakazi wa kituo hicho hawana mikataba rasmi hivyo amemuagiza Mmiliki wa kituo hicho akisimamiwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya Mvomero kuhakikisha wafanyakazi hao wanapatiwa mikataba na kuwasilisha taarifa za mikataba hiyo kwa kiongozi huyo.
"...namuelekeza Mwanasheria wa Halmashauri leo hii awasimamie na kuandaa huo mkataba...baada ya kila mtumishi apate mkataba..."amesema Ndg. Godfrey Mzava.
Katika hatua nyingine, Kiongozi huyo amewataka wataalam wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufunga vifaa vya kutambua viashiria vya uwepo wa moto katika kituo hicho ndani ya siku tatu kuanzia leo Aprili 20, 2024 mafuta ili kusaidia kupunguza hatari ya kutokea kwa moto kituoni hapo.
Awali wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho Bw. Peter Mamilo amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Disemba 2023 na kukamilika Machi 2024 huku akibainisha kuwa mradi umegharimu zaidi ya milioni 300 hata hivyo umeshakamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutoa huduma kwa wananchi. Pia ameongeza kuwa mradi huo utawasaidia wakazi wa Mziha na maeneo jirani kuwapunguzia adha ya kutembea zaidi ya kilometa 35 kufuata huduma ya mafuta maeneo mengine.
Mwenge wa Uhuru 2024 umepokelewa katika kijiji cha Mziha leo Aprili 20 na kuanza kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero huku ukiambatana na Kaulimbiu isemayo Tunza Mazingira na shiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.