Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ametoa maelekezo kwa wazazi na walezi ndani ya Wilaya ya Mvomero kuhakikisha wanawaleta Watoto wao kuripoti shuleni ndani ya wiki moja kuanzia leo ikiwa ni siku 3 tu toka muhula mpya wa shule ufunguliwe kwa shule za awali msingi na sekondari kwa mwaka 2024 nchini Tanzania.
Mkuu wa Wilaya ametoa rai hiyo wakati alipofika kufanya tathmini ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa ya awali na Shule za Msingi pamoja na kuripoti kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2024.
Katika ukaguzi wake alipopita katika Shule ya Msingi Kwamuhuzi, ameridhika na kasi ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali Pamoja na darasa la kwanza huku kwa darasa la kwanza uandikishaji ukiwa umefikia asilimia 83 huku bado wazazi wakihamasika kuandikisha Watoto wao na kuleta matumaini ya kufikia lengo la asilimia 100.
Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa wazazi kuwaandikisha Watoto wao na kutoa maelekezo kwa walimu wa shule hiyo kupokea wanafunzi wapya hata kama hawana sare za shule ili kuwaapa wazazi muda wa kutafuta sare hizo.
Aidha, katika ukaguzi wake kwa Shule ya Sekondari Kumbukumbu ya Sokoine, Mkuu wa Wilaya hajaridhishwa na kasi ya kuripoti kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kwani kati ya wanafunzi 50 waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza shuleni hapo, ni wanafunzi 16 tu ndio walioripoti na kuanza masomo.
Ametoa maelekezo kwa wazazi, walezi, watendaji wa kata na vijiji kuhamasisha na kufichua wanafunziwanaofichwa katika maeneo yao kuripoti shuleni na kuanza masomo kwani elimu ni haki na sio hisani na Watoto wanatakiwa kupata elimu kadri inavyotakiwa na kumchelewesha mwanafunzi masomo ni kumnyima haki yake ya msingi.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshafanya jukumu lake kuleta fedha kujenga miundombinu wezeshi Pamoja na kuondoa ada ili wanafunzi hao wasome, sasa ni jukumu la wazazi kuwapeleka Watoto waanze shule. Mkuu wa Wilaya amesema hatakuwa tayari kuona Watoto wanapoteza haki hiyo ya msingi.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.