Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amemtaka aliyekuwa Mkandarasi wa ujenzi wa kisima cha maji katika kitongoji cha Sokoine Ranchi kulipa madeni yake zaidi ya shilingi milioni 46 anayodaiwa na vibarua wake, mama lishe pamoja na mzabuni.
Mhe. Nguli ametoa agizo hilo Juni 28, mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Sokoine Ranchi alipokwenda baada ya kupokea malalamiko ya wananchi juu ya Mkandarasi huyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema Mkandarasi uyo anatoka kwenye kampuni Selflink limited ambaye inasemekana ni mtumishi wa TANROADS Rukwa. Kwa mujibu wa mkataba Mkandarasi huyo ameshalipwa asilima 90 ya kazi lakini kwa sasa amesimamishwa kuendelea na ujenzi huo.
Aidha, Mhe. Nguli amebainisha kuwa jitihada mbalimbali za kumtafuta zimefanyika ili alipe madeni yake lakini mkandarasi huyo hajajitokeza.
"...nimpe siku tatu huyo msimamizi wa mradi na kampuni yake siku tatu kuyalipa madeni yake mara moja..." amesema Mkuu wa Wilaya.
Sambamba na hilo Mhe Judith Nguli amewataka wananchi kurudisha mali za mkandarasi walizochukua ikiwemo vifaa vya mradi pamoja na gari aina ya Toyota Nissan lenye namba za usajiri T 471 AMK na kuwataka kutojichukulia sheria mkononi.
Kwa upande wao vibarua wanaomdai mkandarasi huyo akiwemo Bw. Juma Daniel amesema alipewa kazi ya kuchimba karo la tenki la maji ambapo malipo yake ni shilingi 290,000 lakini hadi sasa amelipwa shilingi 150,000 tu.
Naye Bi. Halima Seluhinga amesema aliwapangisha chumba kwenye nyumba ya wageni ambapo pesa anayodai ni shilingi 500,000, flemu ya duka 70,000 na baadhi ya vyombo vimechukuliwa na wafanyakazi wa mkandarasi huyo. Aidha, amebainisha kuwa aliamua kulizuia gari la mkandarasi hadi pale atakapolipwa lakini kwa maelekezo ya Mkuu wa Wilaya anarudisha gari hilo.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.