Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mh.Halima Okash ameuagiza uogozi wa Serikali ya Kata ya Mlali kuhakikisha ndani ya siku 7 wawe wameunda Chombo cha ya Watumia Maji ndani ya jamii ili kumaliza kero ya maji katika Kata hiyo.
Agizo hilo la Mkuu wa Wilaya amelitoa hapo jana katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Meneja wa RUWASA wa wilaya hiyo ya kuwa miongoni mwa sababu zinazosababisha ukosefu wa maji ni baadhi ya vijiji kushindwa kufanya uchaguzi kuwachagua wajumbe wa wawakilishi watakaounda Chombo cha watumia Maji katika kata hiyo jambo ambalo limesababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wananchi na viongozi wa serikali katika kata hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka viongozi wa serikali katika kata hiyo hususani wa Kijiji cha Mlali kusimamia vyema rasilimali za umma na kuwashirikisha wananchi katika masuala mbalimbali ya maendeleo ili kuleta utawala bora na uwajibikaji.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ili maendeleo yaweze patikana ni lazima kuwepo na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika utoaji maamuzi.
Katika hatua nyingine, Mh. Halima Okash amepiga marufuku shughuli zote za waganga wa jadi maarufu kama Lambalamba (ramli chonganishi) kufanyika katika eneo lote ndani ya wilaya na atakayejihusisha na maswala hayo au kuwaleta waganga hao kwa ajili ya shughuli hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Hassani Njama amesema miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya kata hiyo ni migogoro ya mara kwa mara kati ya viongozi na wananchi, hivyo ameutaka uongozi wa kata hiyo kujitathmini upya na kumaliza tofauti zilizomo miongoni mwao na kuanza kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta maendeleo katika kata hiyo.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh. Yusuf Makunja, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutoa maelekezo hayo kwa uongozi wa kata hiyo ili kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa eneo hilo zikiwemo za ukosefu wa maji, upungufu wa vyumba vya madarasa na kupata ufumbuzi wa kutafuta eneo la kudumu kwa ajili ya ujenzi wa soko katika kata hiyo.
Mh. Makunja amemuahidi Mkuu wa Wilaya kwamba yeye pamoja na Mkurugenzi, watasimamia yale yote yaliyoelekezwa na Mkuu huyo ili kuweza kumaliza tofauti zote zilizopo katika kata hiyo ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.