Jamii imetakiwa kushikamana kwa pamoja katika kupinga na kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazokiuka haki za mtoto, ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na ajira za watoto, ili kulinda ustawi wa watoto na kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya kuishi, kupata elimu na malezi bora.
Wito huo umetolewa Juni 16, 2025 na Afisa Tawala Wilaya ya Mvomero Bw. Flezier Mang’ula akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kiwilaya yamefanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Manyinga B.
Bw. Mang’ula amesema kuwa mila potofu zimeendelea kuwa chanzo kikuu cha ukiukwaji wa haki za watoto hasa wa kike, jambo ambalo linadumaza maendeleo ya watoto na jamii kwa ujumla.
“…kwahiyo ni vizuri tukaendelea kukemea mila ambayo inamdumaza mtoto” amesema Bw. Mang’ula.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa viongozi wa kijamii na wa kidini kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya haki za watoto na kupinga mila zote zinazowadhalilisha au kuwanyima fursa ya maendeleo.
Kwa upande wao Watoto kupitia risala iliyosomwa wamesema ripoti zinaonesha kuwa matukio ya unyanyasaji kwa Watoto vimeongezeka kutoka visa 12163 mwaka 2022 hadi 15301 mwaka 2023, ubakaji uliongezeka kutoka 6827 kwa mwaka 2022 hadi 8691 mwaka 2023. Ameongeza kuwa matukio ya ukatili kwa mkoa wa Morogoro yameongezeka hadi matukio 976 mwaka 2023.
Naye, mwanafunzi Jackline Eliabe kutoka shule ya Msingi Manyinga A amebainisha aina mbalimbali za ukatili kwa Watoto zikiwemo ukatili wa kijinsia, saikolojia na ukatili wa kimwili aina hizo za ukatili huleta athari za moja kwa moja katika maendeleo ya mtoto.
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 16 ambapo kwa mwaka huu yamepambwa na kaulimbiu isemayo “Haki za Mtoto; Tulikotoka, Tulipo na Tuendako.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.