Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imepongezwa kwa kuonesha juhudi katika kufuatilia marejesho ya mikopo iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia asilimia kumi ya mapato ya ndani.
Pongezi hizo zimetolewa Juni 12, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Halmashauri ya Mvomero imeonesha juhudi kutokana na utaratibu mzuri wa kuwasiliana na vikundi vilivyokopeshwa, kufuatilia maendeleo yao na kuchukua hatua stahiki kwa vikundi vilivyoshindwa kurejesha mikopo kwa wakati.
"...niseme jambo moja na hili lazima niliseme, katika Halmashauri zote ninyi mmechukua hatua zinazoeleweka kuliko watu wengine wote...." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, ameitaka Halmashauri kuendelea kufuatilia kwa karibu na kuwasilisha taarifa ya hatua iliyofikiwa katika ufuatiliaji huo. Hata hivyo, ametoa wiki mbili kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mvomero, Bi. Sia Ngao kuandaa mkakati unaoonesha muelekeo wa malipo ya mikopo iliyotolewa kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa maelekezo na maagizo aliyoyatoa yatafanyiwa kazi kwa wakati.
Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuph Makunja wakati akifungua kikao hicho amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha usimamizi wa mapato ya Wilaya ya Mvomero.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.