Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bi. Loema Peter, amesema kuwa ili wananchi wapate huduma bora ni lazima suala la uwajibikaji litekelezwe kwa dhati, likijumuisha kufika kazini kwa wakati, kuwepo kazini na kufanya kazi kwa bidii.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo Juni 5, 2025 wakati akizungumza na watumishi wa Idara ya Afya kwenye kikao cha kupokea taarifa za maendeleo ya Vituo vya kutolea huduma za Afya kwa Mwezi Mei, 2025, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Bi. Loema Peter ameeleza kuwa nidhamu ya muda na uwepo wa watumishi katika maeneo yao ya kazi ni misingi muhimu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Ili huduma zitoletwe na ziwe ni huduma bora, suala la uwepo wetu kazini, kufika kwa wakati na kufanya kazi ni jambo muhimu sana,” amesema Bi. Loema Peter
Aidha, amewataka Wasimamizi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanakuwa mfano wa kuigwa kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuwasimamia ipasavyo watumishi walioko chini yao, ili kuhakikisha malengo ya Serikali katika kuwahudumia wananchi yanafikiwa.
Sambamba na hilo, amewataka kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora za Afya kwa wananchi huku akibainisha kuwa Serikali imeboresha miundombinu ya Afya kwa kujenga Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati huku ikiboresha na maslahi ya watumishi hivyo, ni wajibu wao kutoa huduma bora.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji huyo amewataka Wasimamizi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya kusimamia miradi ya afya inayotekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa kulingana na fedha iliyotolewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Phillipina Phillipo amesema kuwa Idara imeweka utaratibu wa kufanya vikao vya tathmini kwa kila mwezi ambapo kila msimamizi wa kituo cha Afya anawasilisha taarifa ya kituo chake.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa Afya Ndg. Lubadanja amemshukuru Mkurugenzi kwa maelekezo aliyatoa huku akiahidi kuwa wataenda kuyafanyia kazi.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.