Wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wamepewa siku saba kuhakikisha wamelipa madeni wanayodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD).
Agizo hilo limetolewa Juni 5, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Loema Peter, wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utoaji wa huduma za Afya kwa mwezi Mei ambacho kimewakutanisha Wasimamizi wa Vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo mbalimbali wilayani humo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Bi. Loema Peter amesema kuwa Serikali kupitia MSD imetoa vifaa tiba, dawa pamoja na vitendanishi kwa wakati hivyo kila msimamizi hao wanatakiwa kulipa kwani fedha wanazo huku akitoa siku saba kuanzia Juni 5 hadi Juni 12, 2025 kulipa deni hilo.
"...MSD amekupa huduma ya dawa, Vifaa tiba, vitendanishi halafu fedha zipo kwenye akaunti hujalipa tafadhali ndani ya hizi siku saba hadi tarehe 12 nione fedha zote zimelipwa..." ameagiza Mkurugenzi.
Sambamba na agizo hilo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amewasisitiza kutumia mfumo wa GoT-HoMIS (Government of Tanzania Health Operation Management Information System) katika vituo vyao akibainisha kuwa suala la kutumia mfumo huo ni la lazima kwani ni agizo la Serikali.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.