Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewaasa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuwa na umoja katika utendaji kazi kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwatumikia wananchi na kusogeza maendeleo katika sehemu zao za kazi.
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo katika kikao-kazi cha ndani alichofanya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Serikali wakiwemo Watendaji wa Kata, Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Serikali Vijiji wa Tarafa ya Mvomero kilichofanyika Makao Makuu ya Kata kijiji cha Mvomero Jumatano, 20 Desemba 2023.
Katika Kikao hiko , Mkuu wa Wilaya amewataka kuitumikia dhamana waliyopewa na Serikali kwa kusimama na kufanya kazi kwa pamoja na waache tabia ya baadhi yao kuleta mpasuko kwenye vijiji vyao na badala yake wasikilize na kutatua kero za wananchi kwani wananchi ndio waliowapa nafasi walizokuwa nazo hivi sasa.
Mkuu wa Wilaya amesema ya kwamba amegundua baadhi ya Wenyeviti wa Mitaa wameanza kampeni za chinichini kuwania nafasi za uongozi mapema sana kinyume na utaratibu uliowekwa na Serikali jambo ambalo linaleta mpasuko na kukwamisha baadhi ya shughuli za Serikali hivyo ni vyema wawe wapole kipindi hiki ili kuruhusu viongozi waliopo wamalize muda wao. “Serikali inapenda viongozi wanaoiunganisha Serikali na sio kuigawa, tofauti zetu zisiigawe Serikali”. Alisema Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewataka Watendaji hao kusimamia vizuri miradi ya Serikali iliyo katika maeneo yao ya kazi. Amewata viongozi hao kuhakikisha kwamba miradi yote inayoletwa na Seriikali inasimamiwa ipasavyo mpaka kukamilika kwake kwani Serikali inapeleka fedha sehemu nyingi sana kwa ajili ya miradi mbalimbali hivyo miradi hiyo kuletwa Mvomero ni nafasi ya kipekee.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amesisitiza umihimu wa lishe mashuleni na kuwataka wazazi , walezi pamoja na jamii iahkikishe inachangia lishe mashuleni ili kukuza taifa lenye afya tele. Pia amekemea migogoro ya wakulima na wafugaji na kuwaomba viongozi hao waunge mkono kampeni ya kitaifa ya Tutunzane Mvomero 2023 inayoenda kuwa chachu za migogoro hii kwenye Wilaya ya Mvomero.
Mwisho kabisa Mkuu wa Wilaya amekemea tabia ya baadhi ya Watendaji wa Serikali kutembea na mihuri na kuwaomba wairudishe mihuri hiyo ofisi kwani ina nguvu kubwa na ikitumiwa vibaya ni chanzo cha migogoro ya ardhi.
Alisisitiza pia umuhimu wa watendaji wa Serikali kukaa kwenye vituo vyao vya kazi ili kuhudumia wananchi. Pia alisisitiza kuwa makini na suala la ugaidi pamoja na uvunjifu wa amani. “Ukiona sura ngeni, toa taarifa”
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.