Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amefanya ziara katika Kijiji cha Ng’ungulu kilichopo Kata ya Tchenzema ili kujionea maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia fedha zinazotolewa na Serikali.
Katika mkutano wa hadhara alioufanya katika kijiji hiko, Mkuu wa Wilaya amesisitiza mambo katika nyanja mbalimbali na kutatua baadhi ya kero zinazowakabili wanakijiji hao.
Mkuu wa Wilaya ametaka wananchi kujali na kulinda barabara kwani ndio kiungo kikubwa kwa maendeleo yao. “Tusaidiane kulinda miundombinu yetu.Tutunze na kulinda barabara zetu. Naomba baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuchepusha maji juu ya barabara kwa ajili ya kilimo waache mara moja.”
Mkuu wa Wilaya ameongeza kuwa uchumi wa kijiji hiko unategemea ubora wa barabara hiyo hivyo ni vyema kuilinda kwani kupitia barabara hiyo itawezesha njegere zinazolimwa kwa wingi kijijini hapo kusafirishwa kirahisi kwenda kwenye masoko hasa mjini Morogoro.
Kwa upande mwingine amepongeza walengwa wa TASAF kwa kufanya ukarabati wa kipande cha barabara hiyo ya Tchenzema-Ng’ungulu kwani ni mfano wa kuigwa katika kuiunga mkono Serikali katika kuleta maendeleo.
“Tushirikiane kuondoa maeneo korofi ili tusaidie katika ujenzi wa miundombinu. Nawapongeza sana walengwa wa TASAF, wakati napanda huku nimeona kipande fulani nikaambiwa kimekarabatiwa na walengwa wa TASAF. Naomba tuige mfano wao”
Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Mvomero Mhandisi William Lameck amesema kupitia mradi wa RISE Program ambao ni mradi wa uboreshaji wa barabara za vijijini kwa ushirikishaji na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi , kwenye ujenzi wa barabara hiyo ya Tchenzema-Ng’ungulu, vikundi mbalimbali vitashirikishwa ili kusaidia kulinda barabara za hiyo. Mradi huo unatekelezwa katika mikoa minne(4) ambapo katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Mvomero imepata fursa hii .
Mkuu wa Wilaya pia amekagua ujenzi wa Shule ya Msingi Ng’ungulu ambayo imepata kiasi cha Shilingi Milion 110 kupitia mtadi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa madrasa manne(4). Amewataka walimu kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufyatua matofali mengi Zaidi japo kuna changamoto ya usafirishaji wa vifaa na upatikanaji wa malighafi kama vile mchanga kwa ajili ya ujenzi wa matofali.
“Naomba mwalimu muongeze kasi ya ufyatuaji wa matofali. Nimeangalia kwenye taarifa yenu. Matumizi yenu ya fedha ni mazuri ila ongezeni kasi ya ujenzi ”.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa elimu kwa watoto na kuelekeza uongozi wa Halmashauri uangalie maeneo yenye changamoto ya uhaba wa walimu kuelekezewa walimu. Ameiomba Halmashauri kuweka mazingira rafiki kwa maeneo yasiyofikika kirahisi kujengewa miundombinu wezeshi ambayo itashawishi walimu kubaki katika maeneo yao ya kazi na si kukimbia pindi tu wanaporipoti kwa mara ya kwanza.
Pia amewaasa walimu kuongeza ya kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanahudhuria madarasani kwani kwa ulimwengu wa sasa, ili kumudu kuishi, mwanafunzi anahitaji elimu iliyo bora.
“Serikali imeleta elimu bure mpaka kidato cha sita, mwandae mtoto ili apate kwenda shule aje kukusaidia baadae” , ameongeza hayo wakati akiongea na wazazi kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapo.
Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa lishe kwa jamii na kwa wanafunzi pia. Amewataka wazazi kuchangia chakula mashuleni kupitia kilimo wanachofanya.
“Tuendeleze lishe mashuleni, tutoe vyakula kuimarisha lishe. Wanaume wapeni wajawazito lishe bora. Tukwepe udumavu kwa watoto wetu”.
Kwa upande wa Afya , Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wa Ng’ungulu kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii, CHF ili kupunguza gharama za matibabu zinazokuwa kubwa pindi mtu anapougua akikosa kadi ya uanachama wa mfuko huo.
“Wananchi jiungeni na Bima ya Afya , CHF.Itawapunguzia sana gharama. Ni elfu 30 tu. Ukiwa na familia ya watu 6, mnapata matibau mwaka mzima. Hii ni sawa na kila mtu kuchangia shilingi elfu 5 tu mwaka mzima. Ukiwa na kadi ya CHF, hupati tabu.”
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Mvomero Ndg. Mlenge Lupetulilo amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wamepata fedha kwa ajili ya upimaji na usanifu wa miradi ya maji kwa ajili ya miradi ya maji vijiji mbalimbali . Amewaomba wanakijiji wafanye vikao kupitia viongozi wao na waamue wapi kuna vyanzo vya maji vya uhakika ili wataalam wa RUWASA waweze kufika na kufanya utafiti wa kina ni vipi watavuna maji ya uhakika. Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 23/24 vijiji vya Ng’owo, Ng’ungulu, Muhale na Chohero viko kwenye mpango wa upimaji.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.