Mkuu wa Wilaya ya MVomero Mheshimiwa Judith Nguli amewaahidi Wananchi wa Mkindo kuwa kutakuwa na haki katika usuluhishi wa migogoro ya Wakulima na Wafugaji katika Kata ya Mkindo na maeneo mengine Wilayani Mvomero.
Mkuu wa Wilaya ametoa ahadi hiyo wakati alipofanya ziara kukagua Skimu ya Umwagiliaji ya Mgongola iliyopo Kata ya Mkinda Wilayani humo. Ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bungoma Wilayani Mkindo alipoenda kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi wa Mkindo Jumamosi tarehe 15, Julai 2023.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amesema hafurahishwi na migogoro inayojitokeza mara kwa mara kati ya Wakulima na Wafugaji huku akiagiza wananchi watoe taarifa kwa kufuata ngazi husika ili watu waovu wanaohatarisha Amani katika Wilaya ya Mvomero wabainike na kuchukuliwa hatua mapema.
“Hakuna aliye juu ya sheria. Hatutamfumbia macho mtu yoyote anayehatarisha amani katika Wilaya yetu. Nawaomba wananchi watoe taarifa kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata mpaka Wilaya ili tubaini watu waovu wanaohatarisha amani ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.” Amesema Mkuu wa Wilaya. “Kama unamjua mfugaji anayehatarisha amani peleka jina lake katika ngazi ya Kijiji ili wafanye kazi na Polisi Kata ili haki itendeke ili mkulima alipwe stahiki yake kwa kufuata miongozo ya kisheria. ” ameongeza Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa Wilaya pia amewaasa wafugaji wafuate njia za kisasa za kulisha mifugo ili kuepusha migogoro isiyokuwa na lazima kati ya Wakulima na Wafugaji. Ametoa maelekezo kuwa wafugaji wapewe mashamba ili waweze kupanda majani kwa ajili ya mifugo yao na kuepuka kulisha mifugo katika mashamba ya Wakulima. “Sitaki kuona wafugaji wanalisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima. Tunao wafugaji wa kuigwa hapa Mvomero ambao wamepanda majani kwenye mashamba yao kwa ajili ya mifugo kama Maloroi, Shamba Kubwa. Huwezi kusikia hawa wanasababisha migogoro.Nitakuja kutoa mfano mwenyewe katika kupanda majani hapa.” Ameongeza Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ameiasa jamii ya Wanamvomero kukuemea vitendo vya kiovu vinavyoharibu maadili ya kitanzania. Amewaomba wananchi wafichue watu wote wanaoharibu watoto huku akiahidi kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote watakaobainika kujihusisha na ulawiti wa watoto na kuharibu maadili ya Kitanzania kwa kutoa elimu isiyofaa kwa watoto. “Tayari kuna taasisi moja tumeibaini inafundisha watoto mambo yasiyofaa. Taasisi hii tayari tumeifungia.” Amesema Mkuu wa Wilaya.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.