Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amefanya ziara kutembelea wananchi na kutatua kero zao pamoja na kukagua miradi inayopata fedha katika Kata za Melela, Lubungo, Msongozi na Mangae ikiwa muendelezo wa utaratibu aliojiwekea kila wiki kutekeleza majukumu yake.
Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Kamati ya Usalama , wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Wakuu wa Taasisi za TAWA, TARURA, TANESCO pamoja na RUWASA, Mkuu wa Wilaya amepokea na kutatua kero mbalimbali za wananchi katika kata hizo.
Awali kabla ya kufanya Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kimambila tarehe 22 Agosti , Mkuu wa Wilaya alikagua shule ya Sekondari ya Lubungo iliyojengwa kwa fedha za UVIKO-19 na kujionea ukamilishwaji wa ujenzi wa madarasa ya shule hiyo huku akiagiza mamlaka husika zikamilishe usajili wa shule hiyo kwani wananfunzi wanatembea umbali mrefu sana umbali wa jumla wa kilomita 44 kwenda Shule ya Sekondari Mongola.
Akitoa maagizo hayo, Mkuu wa Wilaya ameitaka Ofisi ya Uthibiti Ubora Wilaya ya Mvomero kuipa kibali shule hiyo ili kuwaondolea wanafunzi hao adha ya umbali pamoja na hatari ya kujeruhiwa au kuuliwa na tembo kwani Kata hiyo ipo karibu sana na hifadhi ya Taifa ya Mikumi na ni njia ya tembo hivyo ni rahisi sana wanafunzi hao kukutana na wanyama hao pindi waendapo au watokapo shuleni.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ametaka kushughulikiwa kwa haraka kwa migogoro ya mipaka iliyopo katika ya Wilaya ya Mvomero na Manispaa na Morogoro huku akimuagiza Afisa Ardhi afanye haraka kuandaa mkutano kati ya viongozi wa pande hizi mbili ili watoe matamko swala la mgogoro huu limalizwe.
Mkuu wa Wilaya pia amewata Watumishi wa Serikali ambao hawaishi maeneo yao ya kazi kurudi haraka katika maeneo hayo kwani wananchi wanahitaji huduma za watumishi hao ziwe karibu muda wote.
Mkuu wa Wilaya pia baadae aliendelea na ziara katika Kata ya Melela ambapo alifanya mkutano wa hadhara na wananchi huku akitaka viongozi kushughulika ngazi ya Kijiji na kata kushughulikia kero za wananchi ambazo zipo ndani ya uwezo wao mapema kabla hazijafika ngazi za juu.
Katika mkutano huo wa hadhara pamoja na mambo mengine, amewataka wananchi kufuata utaratibu pindi wanapohitaji huduma fulani kutoka serikalini kama ununuzi wa ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali au kuunganishiwa umeme kwani wasipofuata utaratibu uliowekwa na Serikali wanajiweka kwenye hatari ya kutapeliwa na kujiwekea wakati mgumu.
Katika kata za lubungo, Melela, Msongozi, Doma na Mangae Mkuu wa Wilaya aliongelea mambo mbalimbali ila dhima kuu ikiwa ni kero zinazosababishwa na wanyama waharibifu aina ya tembo kwani katika kata hizi zote nne, mashamba ya wakulima yamekuwa yakivamiwa na kuliwa hivyo kuwasababishia wananchi hasara kubwa kiuchumi. Pia vifo vingi vimeripotiwa katika maeneo hayo kwa kuwa yanapakana kwa karibu na Hifadhi ya Taifa Mikumi.
Masuala mengine ambayo Mkuu wa Wilaya aliyatatua katika kata hizo ni umeme, elimu, maji, migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na masuala mbalimbali za kijamii.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.