Katika maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika, Watanzania wameaswa kuwa na mioyo ya kujitolea pamoja na uzalendo na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulijenga na kuliendeleza taifa.
Akihutubia Desemba 8, 2024 katika kongamano la miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara sherehe za uhuru lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ualimu Muhonda, Wilayani Mvomero, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Ndg. Saidi Nguya amewahimiza wananchi kuenzi uhuru walioupata kwa kujituma, kushirikiana, na kuchangia maendeleo ya nchi katika sekta zote.
"...utapewa unachopewa lakini lazima tutangulize moyo wa kujitolea ndiyo silaha ya maendeleo yetu..." amesisitiza Ndg. Nguya.
Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyoyatoa mwaka 1988 wakati akizungumza na wazee wa Mkoa wa Tabora, Mwl. Nyerere alisisitiza kuwa "kama tunataka kupata maendeleo ya haraka ni lazima kama nchi tujenge mioyo ya kujitolea".
Aidha, Katibu Tawala huyo amewataka vijana, ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini, kutumia fursa zilizopo kujenga taifa lao kwa moyo wa kujitolea, ubunifu, na uzalendo, huku akisisitiza kuwa roho ya kujitolea ni urithi unaopaswa kudumu kwa vizazi vyote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni ameipongeza na kuishukuru Serikali za awamu zote sita kwa juhudi zilizofanyika hadi sasa kwani nchi imepiga hatua mbalimbali za maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa. Ameongeza kuwa bado mapambano yanaendelea ili kupata uhuru wa kifikra na uchumi ili kujenga taifa la kizalendo.
Naye Diwani wa Kata ya Muhonda Mhe. Rashid Juma ametumia kongamano hilo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ambayo watanzania wanakila sababu ya kumpongeza kwa hilo.
Akitoa neno la shukrani kwa Viongozi na wageni waliohudhuria kongamano hilo mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho cha ualimu Muhonda amesema kupitia kongamano hilo wao kama wanafunzi hususan wa kikazi cha miaka ya 2000 wamejifunza mengi ikiwemo uzalendo.
Sherehe za uhuru mwaka huu 2024 zinatawaliwa na kaulimbiu inayosema "Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo yetu"
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.