Diwani wa Kata ya Mlali Mhe. Frank Mwananziche, ameipongeza Serikali kwa hatua ya kuboresha huduma katika Kituo cha Afya Mlali, akisema juhudi hizo zimeimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza Disemba Mosi, 2024 kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika Kata hiyo Mhe. Mwananziche amesema kuwa maboresho yaliyofanyika yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakumba wananchi, hasa upatikanaji wa matibabu kwa wakati.
"...na sisi wananchi wa Mlali tunakila sababu ya kuthamini mchango mkubwa ambao Serikali imewekeza kwenye eneo letu kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya..." amesema Mhe. Mwananziche.
Aidha, Mhe. Mwananziche ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana katika kuhakikisha kuwa elimu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI inakuwa endelevu huku akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya kina kwa jamii juu ya kinga, matibabu, na kupunguza unyanyapaa kwa waathirika.
Katika hatua nyingine, Diwani huyo amewataka wananchi kuendelea kupokea elimu zinazotolewa na wadau ikiwemo kupima afya zao huku akisisitiza kuwa afya ndiyo mtaji wa maisha.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.