Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amefanya uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Novemba 24, 2023 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Morogoro.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Malima alieleza kuwa Mkoa huo umevuka malengo ya tisini na tano tatu (95, 95, 95) hadi kufikia mwezi Septemba 2023 Mkoa umevuka malengo katika mapambano dhidi ya maambukizi ya UKIMWI kwani Tisini na tano ya kwanza (wananchi wanaotambua hali zao za maambukizi ya VVU baada ya kupimwa ni asilimia 98.8%), Tisini na tano ya pili: (wanaotumia dawa kati ya watu waliogundulika kuwa na VVU ni asilimia 95%) na Tisini na tano ya tatu (inaonyesha kuwa kati ya watu wanaoishi na VVU ambao wanatumia dawa za ARV wamefubaza VVU ni asilimia 95.8%).
Mhe. Kighoma Malima amebainisha kuwa Mkoa huo uliweka malengo yake kuwafikia wananchi na kutoa elimu dhidi ya kutokomeza VVU na UKIMWI kwa makundi mbalimbali ya Vijana.
Jitihada nyingine zilizotumika katika kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo ni pamoja na kutoa ushauri nasaha na upimaji wa hiari, matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa Malima ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika afua za kupambana na UKIMWI ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Jamii iongoze kutokomeza UKIMWI”.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kuwa na mwitikio chanya wa upimaji wa hiari ambapo kumekuwa na ongenezko la watu wanaopima VVU kila mwaka kutoka 226,213 kwa mwaka 2021 mpaka 292,731 kwa mwaka 2022.
Akibainisha ratiba ya wiki ya maadhimisho Mhe. Adam Malima alisema, maadhimisho hayo yanaenda sambamba na Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na ujumbe wa mwaka huu unasema Wekeza kuzuia ukatili wa Kijinsia.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt.Jerome Kamwela amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano alioutoa hadi kufanikisha maadhimisho hayo.
Naye mwakilishi wa Baraza la watu waishio na VVU (NACOPHA) Bw. Emanuel Msinga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo za Afya na kutoa fursa kwa wananchi waishio na VVU kupata mikopo ambayo inasaidia kuendeleza shughuli za kiuchumi.
UKIMWI uligundulika Wilayani Kilosa mwaka 1998 ikiwa ni miaka 35 iliyopita tangu mgonjwa wa kwanza kupatikana Hospitali ya Wilaya ya Kilosa. Hadi sasa jumla ya watu 71,979 wanaishi na VVU Mkoani Morogoro. Kilele cha maadhimisho ya UKIMWI Duniani hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 1 Desemba ambapo kwa mwaka huu kitaifa yatafanyika Mkoani Morogoro.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.