Mfumo wa stakabadhi ghalani umetajwa kuwa mkombozi kwa wakulima wa zao la kakao hapa nchini hususan wakulima wa Mhonda Wilayani Mvomero kwani umeboresha maisha na kuimarisha uchumi wao kwa kuuza zao hilo kupitia mfumo huo kwa bei nzuri sokoni na kwamba umewasaidia kuepuka unyonyaji wa madalali na kupata thamani halisi ya mazao yao.
Hayo yamebainishwa Oktoba 20, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deo Mwanyika wakati wa akizungumza na wakulima wa zao hilo kwenye kitalu cha kakao kilichopo katika Kata ya Mhonda.
Mhe. Mwanyika amesema lengo la Serikali lilikuwa ni kuhakikisha kuwa mkulima wa kakao anapata bei nzuri ili aweze kuinuka kiuchumi. Akielezea mfumo huo amesema kuwa ni mfumo mzuri ambao unamsaidia mkulima kupata bei halisi ya zao hilo huku akisema kuwa changamoto zilizoainishwa na wananchi zitafanyiwa kazi na kutoa wakulima kutoa taarifa kwa wakati ili kuuimarisha mfumo huo.
"...mimi nitoe wito ndugu zangu tutoe ushirikiano ili tuuimarishe huu mfumo, uimarike zaidi kama tunajua kuna watu ambao pengine wanakwepesha hawataki kuleta au wanafanya ujanja ujanja tutoe taarifa kwa muda kwa wakati kwa viongozi wetu..." amesema Mhe. Mwanyika.
Aidha, Mwenyekiti huo amesema wao kama Kamati ya Bunge wanatamani mfumo huo utumike na kwenye mazao mengine kutokana na manufaa yake kwa wakulima kwa sababu pale ambapo walipokuwa hawapati faida sasa wanapata faida.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amesema ziara hiyo imelenga kuangalia mfumo wa stakabadhi ghalani na jinsi unavyowanufaisha wakulima wa zao la kakao huku akimuhakikishia Mwenyekiti wa Kamati hiyo kuwa changamoto zote zilizoainishwa na wakulima zinazohusiana na mfumo pamoja na mauzo Serikali itazifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa mfumo unaimarika zaidi.
Amoeongeza kuwa Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kumkomboa mkulima kwa kuongeza tija ya uzalishaji kwenye eneo dogo huku akibainisha katika maeneo mengi hapa nchini mavuno yameongezeka kutokana na uwepo wa pembejeo za kilimo na kuongezeka kwa bajeti ya kilimo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akitoa neno la shukrani kwa kamati hiyo ya Bunge amesema maelekezo na ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo pamoja na changamoto zilizoelezwa na wakulima zitafanyiwa kazi kuhakikisha kuwa mkulima wa kakao Wilayani Mvomero anapata faida.
Nao wakulima wa zao la kakao waliofaidika na mfumo wa stakabadhi ghalani akiwemo Bw. Boniface Mahenge amesema awali kabla ya mfumowa stakabadhi ghalani walikuwa wanauza kwa bei ya hasara kuanzia shilingi 2000 lakini mfumo huo umesaidia bei kupanda hadi kufikia shilingi 17000 na zaidi. Pia amesema kupitia mfumo huo ameweza kuwaendeleza kimasomo watoto wake wawili na kujenga nyumba ya kisasa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.