Wito umetolewa kwa waandaaji wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki kushirikisha kikamilifu mamlaka za udhibiti wa ubora kama TBS, TMDA, TFDA na WMA ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo kuongeza thamani kwenye bidhaa wanazozalisha na hivyo kuweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa Agosti 2, 2025 na Mhe. Mizengo Kayanza Pinda Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki 2025 ambayo yanafanyika katika viwanja vya Mwl. J. K. Nyerere vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Pinda amesema kuwa lengo la kuwashirikisha mamlaka hizo kuona namna wajasiliamali hao wanavyozalisha bidhaa zao na kuwasaidia kuongeza thamani katika bidhaa hizo ili kurahisisha katika upatikanaji wa masoko ya uhakika.
“…wakati wa maonesho kama haya tuombe mamlaka zile ambazo zimepewa jukumu la kusimamia ubora wa bidhaa mbalimbali tuzifanye kuwa sehemu ya Mikoa ya Kanda hii ya Mashariki…” amesema Mhe. Pinda.
Aidha, Waziri Mkuu huyo Mstaafu amewapongeza Wajasiliamali wa Kanda ya Mashariki kwa kuendelea kuboresha bidhaa zao hali inayowaongezea uhakika wa masoko.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Mwenyekiti wa Maonesho hayo 2025 Mhe. Abubakar Kunenge amesema kuwa maonesho ya mwaka huu yanalenga kuonesha kwa vitendo mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akitoa rai kwa wananchi kutembelea katika maonesho hayo ili waweze kujifunza mbinu na Teknolojia za kisasa za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amebainisha kuwa kwa mwaka huu wakulima, wafugaji, wavuvi pamoaja na Wananchi watapata elimu ya biashara kuhusiana na shughuli zao kwenye banda maalum la B2B yaani Business to Business. Banda hilo litakuwa na wataalam wa kutoa mafunzo kwa wananchi ambayo itawasaidia kuongeza tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
Maonesho ya Nane nane Kanda ya Mashariki yalianza Agosti 1 na yatahitimishwa Agosti 8.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.