Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewataka Maafisa Ugani wa Wilaya hiyo kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya ya uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi Wilayani humo.
Mhe. Nguli ametoa wito huo Agosti 15, 2024 wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Vishikwambi na Sare za Maafisa ugani hao iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira kwa maafisa ugani ili kuhakikisha kuwa wanatimiza majukumu yao ya kuwahudumia wakulima na wafugaji. Hivyo, amewataka kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao huku akisema utendaji kazi wao mzuri ni njia moja wapo ya kurudisha shukrani kwa Serikali.
“...vile utakavyofanya kazi kwa bidii, ndivyo utakavyomlipa Mhe. Rais...” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Judith Nguli amebainisha kuwa vifaa hivyo vitarahisisha utekelezaji wa kampeni ya Tutunzane Mvomero.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Mvomero Mhe. Theresfoli Jaka amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi na watumishi wa Mvomero. Aidha, amewataka maafisa ugani hao kuvitunza vifaa walivyopatiwa ili vilete manufaa katika kazi zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Mohammed Longoi amesema Wilaya hiyo imepokea Vishikwambi 99 pamoja na Sare 102 za maafisa ugani wa Wilaya hiyo huku akibainisha kuwa vifaa hiyvo vimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ya kuhakikisha kuwa huduma za ugani zinaboreshwa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.