Kampeni ya Tutunzane, ambayo inalenga kuimarisha maelewano na ustawi kati ya wakulima na wafugaji, sasa imeanza kuhimiza matumizi ya mbinu za kisasa za ufugaji katika Wilaya ya Mvomero. Kampeni hiyo pia imevutia wafugaji wengi na kuwapatia elimu juu ya faida za kuachana na mifumo ya ufugaji wa kuhamahama na badala yake kutumia mbinu za kisasa zinazoongeza tija na kupunguza migogoro ya ardhi.
Hayo yamebainishwa Januari 25, mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli akizungumza na Viongozi pamoja na Wananchi kwenye mkutano wa mafanikio ya miaka miwili ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilayani humo uliofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Mvomero.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa kampeni hiyo imekuwa mkombozi wa wafugaji hususan wakati wa kiangazi ambapo wafugaji wamehamasika kumiliki ardhi, kulima malisho kuchimba visima ili kuendelea kuwa na uhakika wa malisho ya mifugo yao kwa vipindi vyote vya mwaka.
Aidha, ameongeza kuwa kwa wakulima waishio karibu na hifadhi wamehamasika kulima mazao ambayo ayaharibiwi na wanyama kama tembo likiwemo zao la ufuta, jambo hilo limechangia kuongeza vipato kwa wakulima hao kupitia uzalishaji wa ufuta.
Sambamba na hilo, Mhe. Nguli amesema Rais Samia ataendelea kutoa mbegu kwa ajili ya mashamba 1200 ya wafugaji pamoja na uchimbaji wa visima 5 vya wafugaji na visima 64 kwa ajili ya wakulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi - CCM Wilaya ya Mvomero Mhe. Michael Jaka amesema kuanzishwa kwa Kampeni ya Tutunzane Mvomero ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ambapo chama kimeielekeza serikali kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji huku akimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kampeni hiyo matokeo yake yanaonekana kwa vitendo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mvomero Mhe. Jonas Van Zeeland amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuja na wazo la kampeni hiyo ambayo sasa mvomero imekuwa mfano wa utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.