Kamati za huduma ya mikopo ya asilimia 10 ngazi ya kata wilayani Mvomero zimetakiwa kuhakikisha zinatenda haki katika mchakato wa kupendekeza vikundi vyenye sifa ya kupata mikopo hiyo.
Agizo hilo limetolewa Oktoba 22, 2024, na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli, wakati akifungua mafunzo kwa kamati za huduma ya mikopo ngazi ya kata kwa tarafa za Mgeta na Mlali, yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mzumbe.
Mhe. Nguli amesisitiza umuhimu wa kamati hizo kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha mikopo inawanufaisha wananchi wote bila upendeleo. Amesema mikopo hiyo inapaswa kuelekezwa kwa vikundi vyenye sifa na uwezo wa kurejesha mikopo ili kufikia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa Wilaya.
Aidha, amewataka wajumbe wa kamati kuwa waadilifu na kutanguliza maslahi ya umma, huku akionya dhidi ya vitendo vya rushwa na upendeleo vinavyoweza kuathiri mchakato wa utoaji mikopo.
Naye, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Mashaka Malole amesema Halmashauri hiyo imetenga zaidi ya shilingi milioni 694 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na wenye ulemavu vyenye sifa ya kupata mikopo hiyo. Aidha, amebainisha baadhi ya sifa za kupata mikopo hiyo zikiwemo kuunda vikundi kuanzia watu watano, umri wa miaka 18 hadi 45 kwa vikundi vya vijana pia vikundi hivyo vinatakiwa viwevimesajiliwa.
Kwa upande wake Bi. Angel Charles akiwakilisha kundi la watu wenye ulemavu ameishukuru Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fursa kwa kundi hilo kupata mikopo ya 10 inayotolewa na Halmashauri huku akitoa wito kwa kundi hilo kujitokeza kuchukua mikopo hiyo ambayo itasaidia kuinua hali zao za kiuchumi.
Akizungumza wakati akihitimisha mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Sia Ngao amewashukuru Watendaji wa Kata waliohudhuria mafunzo hayo na kuwataka kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii wa Kata ili kupata vikundi vyenye tija.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za mikopo katika kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, haki, na uwajibikaji, ili kufikia malengo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.