Kamati ya Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Mussa Ali Mussa, leo Januari 14, 2025 imefanya ziara ya kukagua miradi inayopendekezwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru 2025 wilayani Mvomero. Ziara hiyo imelenga kujiridhisha juu ya utekelezaji wa miradi hiyo, kufuatilia thamani ya fedha iliyotumika na kutoa maelekezo muhimu kwa ajili ya kuboresha utekelezaji.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Katibu Tawala huyo amesisitiza umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi. Aidha, amewaelekeza watendaji kuhakikisha miradi inazingatia muda wa utekelezaji, ubora na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Katika ziara hiyo, kamati imekagua miradi mbalimbali ikiwemo ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Mazingira na uwezeshaji wa vijana. Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja zahanati ya Kijiji cha Mlandizi, mradi wa maji Mangae, Kilimo misitu, mradi wa uzalishaji wa mbegu za mahindi (IFFA SEED CO.LTD), ujenzi wa bweni, chumba cha darasa na choo matundu 13 shule ya Sekondari ya Doma.
Pia, kamati hiyo imetembelea mradi wa Usafirishaji wa abiria na mizigo wa kikundi cha Melela Youth na kiwanda kidogo cha kuchakata bidhaa za ngozi pamoja na eneo la mapokezi na eneo la mkesha.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.