Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewataka Askari wa Jeshi la Akiba kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya usalama katika vita dhidi ya madawa ya kulevya ambayo ni tishio kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.
Mhe. Nguli ametoa kauli hiyo Novemba 21, 2024 wakati akifunga mafunzo ya Jeshi la Akiba kundi la 9 mwaka 2024 ambapo kwa mwaka huu yamefanyika katika Tarafa ya Mlali.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa jeshi hilo kuchukua hatua madhubuti za kuzuia biashara haramu ya madawa ya kulevya ikiwemo bangi na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria ili kuwa na Taifa lenye ustawi.
Aidha, amesema kuwa madawa ya kulevya siyo tu yanaharibu maisha ya vijana, bali pia yanachangia ongezeko la uhalifu na kudhoofisha uchumi wa nchi.
"...kikubwa mkazuie madawa ya kulevya...madawa ya kulevya yanaharibu Taifa, yanaharibu wananchi kiakili ..." amesema Mkuu wa Wilaya.
Sambamba na hilo Mhe. Nguli amewataka Askari hao kutojihusisha na vitendo vya uharifu bali watumie mafunzo waliyopata kuzuia uharifu na kulinda amani.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewataka wagombea wa vyama vya Siasa ambao wanafanya kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024 kuhakikisha kuwa wanafanya kampeni hizo bila kuvunja sheria zilizowekwa na kwamba Serikali itamchukulia hatua za kisheria kwa atakaye kiuka.
Kwa upande wake Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Mvomero amesema mafunzo hayo hufanyika kila mwaka ambapo kwa mwaka huu 2024 yamefanyika katika Tarafa ya Mlali huku yakitarajiwa kufanyika Tarafa ya Turiani mwaka ujao. Aidha, ameongeza kuwa wahitimu wa mwaka huu wapo 149 kati yao wanaume ni 96 na wanawake 50 huku wengine 13 wakishindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa upande wao wahitimu wa mafunzo hayo kupitia Risala iliyosomwa mbele ya Mkuu wa Wilaya wamesema mafunzo hayo yalianza Julai Mosi, 2024 yakiwa na wanafunzi 159 lakini waliofanikiwa kuhitimu ni 146. Aidha, wamewasilisha ombi kwa Serikali wakiomba kupatiwa mikopo ili waweze kujishughulisha na ujasiriamali.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.