Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ametoa wito kwa jamii kushirikiana kupaza sauti ili kukemea vitendo vyote vya ukatili vikiwemo mauaji, ukatili wa kijinsia pamoja na suala la mmomonyoko wa maadili lengo likiwa ni kuijenga jamii bora.
Mhe. Nguli ametoa wito huo Juni 18, 2014 wakati akizungumza na wananchi kwenye Baraza la Eid la Wilaya lililofanyika katika kijiji cha Bwage, Kata ya Mziha.
Mkuu uyo wa Wilaya amebainisha kuwa matukio ya ukatili yameongezeka lakini Serikali inaendelea kuongeza bidii kupambana ili kukomesha vitendo hivyo vya ukatili Wilayani humo, hivyo ametoa wito kwa jamii kukemea vitendo hivyo.
"Tunapaswa kupaza sauti wote kwa umoja wetu kukemea mambo haya..." amesema Mhe. Judith Nguli.
Aidha, Mhe. Nguli ametoa wito kwa wananchi kutilia mkazo suala la elimu ya malezi kwa watoto wao ikiwemo elimu ya dini ambayo inamjenga mtu kuwa na hofu ya mungu pamoja na elimudunia.
Naye, Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Shekhe Juma Mndolwa amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vinahatarisha amani na utulivu uliopo hapa nchini hivyo hakuna budi wananchi kuvipiga vita. Aidha, ametoa wito kwa wazazi, walezi, walimu wa madrasa pamoja na mashekhe ngazi ya Kata Wilayani humo kusimamia maadili kuanzia ngazi ya familia.
Kwa upande wake Katibu wa Barala Kuu la Waislam Tanzania - BAKWATA kata ya Mziha Shekhe Shabani Mganga amebainisha changamoto zinazokabili baraza hilo zikiwemo ukosefu wa Msikiti wa Wilaya pamoja na ukosefu wa ofisi ya BAKWATA Wilaya.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.