Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ametoa wito kwa Kamati za huduma ya mikopo ngazi ya Kata za Tarafa ya Turiani na Mvomero kuhakikisha kuwa haki inatawala bila upendeleo wakati wa mchakato wa kupata vikundi vyenye sifa ya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.
Akizungumza Oktoba 23, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa kamati hizo yaliyolenga kuwajengea uelewa juu ya masuala ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, Mhe. Nguli amesema kuwa ni muhimu kila kundi lipate fursa sawa ya kupata mikopo ili kuwezesha maendeleo endelevu.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa utoaji wa mikopo kwa wananchi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020 - 2025 ya Chama cha Mapinduzi - CCM Ibara ya 23 na 24 ambapo CCM iliahidi kupambana na umaskini pamoja na kuwawezeshawananchi kiuchumi.
"Kikubwa Haki ikatawale bila upendeleo" amesema Mhe. Nguli
Aidha, Mhe. Nguli amewasisitiza Wajumbe wa kamati hizo kutoa elimu na ushauri kwa vikundi ili vianzishe miradi inayozalisha na yenye tija kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia wanakikundi kumudu marejesho ya mikopo waliyoiomba.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri Bi. Sia Ngao amesema kwa mujibu wa muongozo mpya wa utoaji wa Mikopo ya asilimia 10 umezielekeza Halmashauri kuwa na Kamati za mikopo ngazi ya Kata kwa kuwa ngazi hiyo ndiko vikundi vingi vinapatikana huku akibainisha lengo la kuundwa kwa Kamati hizo ni kuwasaidia maafisa maendeleo ya jamii katika usimamizi wa mikopo.
Kamati hizo za Mikopo ngazi ya Kata zinaundwa na Watendaji wa Kata, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata, Watendaji wa Vijiji, Maafisa Ugani, Waratibu wa elimu ngazi ya Kata na Askari Kata.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.