Divisheni ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imepongezwa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa Serikali wa GoT-HoMIS, hatua inayodhihirisha ufanisi wa usimamizi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya.
Pongezi hizo zimetolewa Julai 9, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw. Paulo Faty wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa utoaji huduma za Afya kwa mwaka 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mkurugenzi huyo amsema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri baina ya viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya na watendaji wa idara ya afya ngazi ya wilaya huku akiwapongeza kwa kuvuka lengo kwa asilimia 127.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa, hadi kufikia mwisho wa mwezi Juni 2025, Idara ya Afya ilikuwa imekusanya zaidi ya asilimia 127 ya lengo la mapato ya ndani yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia mfumo wa GoT-HoMIS.
Sambamba na pongezi hizo Bw. Paulo Faty amewataka kuendelea kutoa huduma bora za Afya huku akiwasihi kuwa na lugha za staha pindi wanapowahudumia wateja wao kwani kumekwa na malalamiko kwa baadhi ya watoa huduma za Afya wamekuwa wakitoa lugha zisizo za staha na kwamba Serikali haitasita kuwachukulia hatua.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Dkt. Phillipina Phillipo amesema mfumo wa GoT-HoMIS umeboresha uwazi, ufuatiliaji na udhibiti wa mapato, na hivyo kusaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa idara ilijiwekea malengo ya kukusanya shilingi milioni 479,000,000 kupitia mfumo huo ambapo hadi kufikia Juni 29, 2025 wamefanikiwa kukusanya shilingi milioni 607,463,534 ambayo ni sawa na asilimia 127.
Kwa upande wao, baadhi ya waganga wafawidhi kutoka vituo vya afya na zahanati walieleza kuwa mafanikio hayo pia yametokana na mafunzo ya mara kwa mara kuhusu matumizi ya mfumo huo pamoja na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa viongozi wa afya ngazi ya wilaya.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.