Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno P. Mwageni amewataka wauguzi na matabibu kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa ili kuwasogeza karibu na huduma za hospitali kwani kutoa huduma mbaya na kutowasikiliza wagonjwa ni chanzo cha kuwaweka mbali na huduma hizo na kuwafanya wakimbilie kwa waganga wa kienyeji.

Mwl. Mwageni ameyasema hayo mapema Februari 13, 2024 wakati akizungumza na maafisa Afya, matabibu na wauguzi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyopo ukanda wa Mlali, Mgeta na Melela akiwa na lengo la kuwakumbusha wajibu wao katika zoezi la chanjo ya surua na rubella kwa watoto wenye umri wa miezi 9 na chini ya miaka mitano litakalofanyika kuanzia tarehe 15.02.2024 mpaka tarehe 18.02.2024 katika Vituo 75 vya kutolea huduma za Afya vilivyopo katika Wilaya hiyo.

Kampeni hiyo ina lengo la kuchanja watoto wapatao 52,000 katika Wilaya ya Mvomero. Aliwataka waganga wa Vituo vya kutolea huduma za Afya kutangaza huduma hiyo kwa njia ya vipaza sauti katika maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko. Mkurugenzi huyo ameahidi kutoa zawadi kwa Kituo cha kutolea huduma ya Afya kitakachofanya vizuri katika uchanjaji na kuvuka lengo la asilimia 100.

Aidha, Mwl. Linno alivitaka Vituo vinavyopokea fedha za miradi kutoka Serikali Kuu, Wafadhili na Makusanyo ya fedha za papo kwa papo na CHF kuwa makini katika matumizi ya fedha hizo na kuagiza zitumike kadri maelekezo yanavyotaka.


Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji huyo amevipongeza Vituo vya kutolea huduma za Afya kwa kukusanya vizuri mapato kwa kutumia Mfumo wa GoTHOMIS. Pia ameelekeza Vituo hivyo kutumia Mfumo wa NEST katika kufanya taratibu za Manunuzi katika Ngazi ya Makao Makuu na Vituoni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikao hicho Ndg. Jackson Nyaonge alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kwa kutoa maelekezo na kuahidi kusimamia chanjo na kuvuka lengo la asilimia 100.
Baada ya kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji alikagua mradi wa vyoo, shimo la kutupia kondo la nyuma, miradi hii imejengwa kwa fedha za EP4R kiasi cha Sh. 54,000,000 na jengo la kuhifadhia maiti.



MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.