Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Mwl. Linno Mwageni ameonyesha kuridhishwa na hatua kubwa zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Endelevu wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (SRWSS) katika vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, iliyofanyika Januari 16 na 17, 202, Mwl. Linno amesema kuwa mradi huo ni suluhisho muhimu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na mazingira bora katika vituo vya afya, ambavyo ni sehemu muhimu ya kuboresha huduma kwa wananchi wa Mvomero.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia kikamilifu miradi kama hii ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi kwa muda mrefu. Pia ametoa wito kwa wasimaizi wa vituo hivyo kuhakikisha wanapanda miche ya mazao ya kimkakati kama vile karafuu, Kokoa na Chikichi kuzunguka eneo la kituo.
Mradi wa SRWSS unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama vijijini ukiambatana sambamba na ujenzi wa vyoo bora pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka katika ngazi ya kaya na taasisi zote zilizopo katika vijiji 45 vya wilaya ya Mvomero.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Dkt. Philipina Philipo amesema Halmashauri imepokea jumla ya kiasi cha shilingi 490,118,231.39 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafi katika vituo 7 vya kutolea huduma za Afya kwa awamu mbili.
Awamu ya kwanza Halmashauri ilipokea kiasi cha Tsh. 238,848,519.12 na Tshs. 160,666,666 sawa na asilimia 67.26% ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa miundombinu ya usafi wa mazingira katika Zahanati ya Madizini, Lusanga na Kituo cha Afya Mlali na Tshs. 78,181,853.12 sawa na asilimia 32.73% ya fedha zilitumika katika usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi pamoja na uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo bora na matumizi ya vibuyu chirizi katika ngazi ya kaya.
Aidha, ameongeza kuwa kwa awamu ya pili Halmashauri ilipokea kiasi cha Tsh. 251,269,712.27 ambapo Tsh. 200,000,000 sawa na 79.59 % zimeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya usafi katika vituo 4 vya kutolea huduma za Afya ambavyo ni Kituo cha Afya Mvomero, Kituo cha Afya Mgeta, Zahanati ya Kidudwe na Zahanati ya Mikongeni. Kiasi cha Tshs. 51,269,712.27 sawa na 20.40 % zimetumika katika shughuli za usimamizi wa mradi, uratibu wa zoezi la uhamasihaji wa ujenzi wa vyoo bora na matumizi ya vibuyu chirizi.
Halmashauri imefanikiwa kuvuna fedha kiasi cha Tsh. 633,319,750 baada ya kutekeleza mradi huu kwa ufanisi mkubwa. Fedha hii itaendelea kuboresha miundombinu ya usafi wa mazingira kwenye vituo vingine vya kutolea huduma za afya.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.