Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni ametoa agizo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo ngazi ya Kata kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, itolewe kwa kuzingatia vikundi vinavyoonyesha uwezo wa kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mwl. Linno ametoa agizo hilo Oktoba 03, 2024 wakati akifungua Semina ya Muongozo mpya wa utoaji Mikopo ya asilimia 10 kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amewasisitiza Maafisa hao umuhimu wa kufanya uchambuzi wa kina wa vikundi vinavyoomba mikopo, ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinaelekezwa kwa wale wenye mipango thabiti na inayotekelezeka.
"...ninachotaka tukifanye tuviandae vikundi vyenye tija..." amesema Mwl. Linno.
Aidha, Mwl. Linno amewaelekeza Maafisa Maendeleo ya Jamii hao kufuatilia matumizi ya mikopo hiyo ili kuhakikisha kuwa imetumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kutoa matokeo yaliyotarajiwa, hususan katika kuinua hali ya kiuchumi ya wanufaika na jamii kwa ujumla.
Naye, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Bi. Sia Ngao wakati akitoa neno la shukran kwa Mkurugenzi huyo amesema watayafanyia kazi maneno aliyoyatoa huku akimuahidi kutulia mkazo katika zoezi la mchakato wa upembuzi wa vikundi ili kupata vikundi ambavyo vitakuwa vya mfano katika Mkoa huo.
Semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo juu ya mbinu bora za usimamizi wa mikopo, ufuatiliaji wa miradi na namna ya kuwajengea uwezo wanufaika wa mikopo ili kuhakikisha wanapata mafanikio makubwa.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.