Watendaji wa Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wametakiwa kuwaelimisha Wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa uwepo wa chakula shuleni ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchangia mpango huo unaolenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi. Elimu hiyo itasaidia kuongeza uelewa juu ya mchango wa chakula katika kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi, kuongeza umakini darasani na kuboresha ufaulu wa masomo.

Wito huo umetolewa Januari 19, 2026 na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya hiyo Mwl. Bruno Sangwa wakati wa kikao cha kamati ya lishe Wilaya kilichofanyika katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya.

Mwl. Sangwa amesisitiza kuwa chakula shuleni ni nyenzo muhimu ya kuwafanya wanafunzi kubaki shuleni muda wote wa masomo bila usumbufu wa njaa, hali inayochangia kupunguza utoro na kuongeza nidhamu. Aidha, ameeleza kuwa pale wazazi na walezi wanapopata elimu sahihi, huwa tayari kuchangia kwa hiari kupitia michango ya chakula au fedha kulingana na makubaliano ya jamii husika.


Aidha, ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Watendaji hao, kamati za shule na wazazi ni nguzo muhimu ya kufanikisha mpango wa chakula shuleni. Kupitia uelewa huo jamii itaweza kuelewa wajibu wake katika kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora inayowawezesha kusoma kwa afya na ari.
Kwa upande wake Afisa lishe Hospitali ya Wilaya ameeleza kuwa Halmashauri ilipanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 59,843,017 kwa kipindi cha mwezi Julai – Disemba 2025 ambapo kila mtoto alitengewa shilingi 1925, Halmashauri ilitumia shilingi milioni 61,465,904 sawa na asilimia 102 huku akibainisha kuwa kila mtoto amepata kiasi cha shilingi 1977.

Nao baadhi ya Watendaji wa Kata akiwemo Mtendaji wa kata ya Mzumbe Amasha Mwamba ameishukuru Halmashauri kwa kuanda kikao hicho huku akiahidi kuwa wataendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha kuwa Wilaya ya Mvomero inakuwa kinara katika suala la lishe.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.