Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Mwl.Linno Mwageni amewaagiza maafisa kilimo ngazi ya Kata na Vijiji katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanaratibu na kuanzisha mashamba darasa ya mazao yanaolimwa zaidi kwenye eneo husika katika kila shule ya msingi na sekondari ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza Novemba 19, 2024 wakati wa kikao kazi cha wadau wa kilimo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri, Mwl. Linno amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kilimo cha kisasa tangu wakiwa wadogo, ili kuwaandaa kwa maisha ya kujitegemea na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa tija.
"...jamani shule zote za msingi na sekondari lazima ziwe sehemu ambazo kunakuwa na mashamba darasa..." amesema Mwl. Linno
Ameongeza kuwa mashamba darasa hayo pia yatawezesha jamii zinazozunguka shule kujifunza mbinu bora za kilimo kupitia mafunzo yatakayokuwa yakitolewa na walimu kwa kushirikiana na maafisa kilimo.
Aidha, amelipongeza shilika la SUGECO (Ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine) kwa kuja na mradi ambao utawainua vijana kiuchumi kupitia kilimo huku aliahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa Vijana wa Halmashauri hiyo wanajikita kwenye kilimo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa YEFFA (Youth Entrepreneurship for future of food and agriculture) Bi. Jacqueline Jonathan kutoka shirika la SUGECO amesema kuwa mradi huo una lengo la kuimarisha ushirikishwaji na uwezeshwaji wa vijana katika kuzalisha ajira kupitia sekta ya kilimo biashara.
Mradi umefadhiliwa na Mastercard Foundation na utadumu kwa kipindi cha miezi 36(miaka 3) ambapo umeanza rasmi Sept 2024 - Aug 2027.
Bi. Jacqueline ameongeza kuwa mazao yaliyochaguliwa katika mradi huu ni Alizeti, Mahindi, Maharahe, Soya, Mpunga na mazao ya bustani. Hata hivyo, amesema matarajio ya mradi huu ni kupata kanzi data yenye taarifa kamili za vijana wanaojishughulisha kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo na sekta nyingine ili kuboresha ushirikishwaji na uwezeshwaji kupitia program mbalimbali za maendeleo katika sekta ya kilimo hapa nchini, mradi huu pia utawanufaisha vijana 17500 wa Wilaya ya Mvomero.
Mpango huu unakuja wakati ambapo serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya kilimo cha kisasa ili kufanikisha lengo la kujitosheleza kwa chakula na kuongeza pato la taifa.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.