Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Mwl. Linno Mwageni amewataka mafundi na wazabuni wote ndani ya halmashauri hiyo kuhakikisha wanajisajili kwenye Mfumo mpya wa Ununuzi Umma NeST ili kushiriki kwenye fursa mbalimbali za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Mwl. Linno ameyasema hayo Novemba 18, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma - NeST kwa Mafundi na Wazabuni wa Halmashauri hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema mfumo wa NeST ni nyenzo muhimu iliyowekwa na serikali ili kuimarisha uwazi, ufanisi, na uadilifu katika manunuzi ya Umma.
"...Mafundi na wasambazaji wa bidhaa tujisajili kwenye mfumo ili pesa zinazoingia ndani ya Wilaya yetu basi tuzifanyie kazi..." amesisitiza Mwl. Linno.
Aidha, ameongeza kuwa usajili kwenye mfumo huo ni sharti la kisheria kwa watoa huduma wote wanaotaka kushiriki katika zabuni za serikali huku akibainisha kuwa kutokujisajili kutawazuia mafundi na wazabuni kupata nafasi ya kushiriki kwenye miradi mikubwa inayofadhiliwa na serikali katika Wilaya hiyo.
Sambamba na hilo, Mwl. Linno amesema Halmashauri itafanya mpango ea kuhakikisha kuwa mafundi wote wa Wilaya hiyo wanapatiwa vyeti vya taaluma ya ufundi ili waweze kutambulika zaidi lakini pia vyeti hivyo vitawasaidia kujisajili kwenye mfumo huo wa NeST.
Kwa upande wake, Afisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo Bi. Aimana Nkya amewahakikishia watoa huduma kuwa mfumo wa NeST utarahisisha mchakato wa malipo na zabuni, huku ukipunguza changamoto za urasimu zilizokuwepo awali. Hata hivyo, amewataka kutekeleza miradi kwa ubora unaotakiwa na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Naye, Mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri Bw. Michael Mangoli amewataka wasambazaji wa bidhaa kuhakikisha kuwa wanafikisha vitendea kazi kwa wakati ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Nao, mafundi waliohudhuria mafunzo hayo wameishukuru Halmashauri kwa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kupata fursa za kutekeleza miradi ya Serikali. Aidha, wameomba mchakato wa vyeti ufanyike haraka ili waweze kutambulika rasmi.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.