Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni amekabidhi pikipiki mpya nne kwa Idara ya Afya kwa lengo la kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za chanjo pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya usafi na mazingira katika vituo vya kutolea huduma za Afya katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki hizo iliyofanyika Januari 16, 2025 katika ofisi za Halmashauri, Mwl. Linno amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa haraka na ufanisi zaidi.
"...Pikipiki hii unaweza ukakiona ni chombo kidogo sana lakini ikifanya kazi zilizotarajiwa, hii italeta matokeo makubwa sana hasa katika sekta ya chanjo na masuala ya usafi..." amesema Mwl. Linno.
Aidha, amemtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa anawasimamia watumishi waliopokea usafiri huo ili watumie vyombo hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba atakaye kiuka atachukuliwa hatua ikiwemo kunyang'anywa.
Naye, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Philipina Philipo amesema pikipiki mbili zitatumika katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya usafi wa mazingira katika Kata za Mlali na Dakawa, pikipiki nyingine mbili zitatumia katika masuala ya chanjo ambapo moja itatumika kwa ngazi ya CHMT (Timu ya usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za Afya ngazi ya Halmashauri) na nyingine kituo cha Afya Mgeta.
Kwa upande wao baadhi ya watumishi waliokabidhiwa pikipiki hizo akiwemo Afisa Afya wa Kata ya Dakawa Bi. Irene Mtenji amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji, Mganga Mkuu wa Wilaya kwa kuhakikisha kuwa watumishi hao wanapata usafiri. Aidha, amesema usafiri huo utasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kutokana na kuwa baadhi ya maeneo kutofikika kwa urahisi.
Naye, Afisa Afya Bw. Benson Peter amesema pikipiki hizo zitasaidia katika kusimamia na kuratibu shughuli za afua za chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.