Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli, amezindua rasmi mabirika ya kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Kibaoni Kata ya Melela huku akieleza kuwa mradi huo unaakisi kwa vitendo kampeni ya Tutunzane inayolenga kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima kwa kuimarisha upatikanaji wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo hususan wakati wa kiangazi.
Akizungumza Juni 18, 2025 wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Nguli amesema kuwa mabirika hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima kuhakikisha wafugaji wanapata huduma bora kwa mifugo yao, hasa katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji na malisho.
Aidha, amewataka wafugaji kuyatunza mabirika hayo na kuhakikisha yanatumika kama yalivyokusudiwa ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima hasa wakati wa kiangazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la WamiRuvu Mhandisi Elibariki Mmasi amesema kuwa ili kutimiza adhma ya Serikali ya utunzaji wa mazingira pamoja utekelezaji wa Kampeni ya Tutunzane Mvomero ujenzi wa mabirika hayo utanufaisha mifugo 669000 na kaya 19389.
Aidha, ameongeza kuwa Bodi hiyo imekamilisha uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vinne ambapo jumla ya hati za mfano 400 zimeandaliwa.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji Bi. Rosemary Rwebugisa amesema kuwa Wizara ya Maji imekuwa ikitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020/2025 ambapo imeelekeza kuwa ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji maeneo ya Vijijini ufikie asilimia 85 na mijini asilimia 95 huku akibainisha kuwa hadi sasa upatikanaji wa maji Vijijini umefikia asilimia 83.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.