Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amezindua rasmi Baraza la Biashara la Wilaya likiwa na lengo la kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa maendeleo ya jamii na kiuchumi.
Akizungumza Mei 30, 2024 wakati akizindua baraza hilo kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo amesema Baraza hilo linajumuisha sekta za Umma na binafsi kujadili kwa pamoja masuala ya kimkakati katika kuboresha maslahi ya wafanyabiashara Wilayani humo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amebainisha fursa mbalimbali ambapo wamewataka wafanyabiashara kujitokeza kuwekeza katika Wilaya hiyo, miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na kilimo cha mazao ya biashara yakiwemo mazao ya kakao, karafuu, mpunga, fursa za ufugaji na viwanda.
“...unaruhusiwa kuja Halmashauri ukauliza utaratibu, ukapewa muongozo wa namna sahihi ya kutumia hizo fursa za Halmashauri yako...” amesema Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine, Mhe. Nguli ametoa rai kwa wafanyabiashara kuacha tabia ya kuchepusha mapato huku akibainisha kuwa kitendo hicho kinapunguza mapato ya Halmashauri.
Naye Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Nsubisi Kapula ameeleza vipaumbele vya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025 upande wa biashara ikiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi Mlali, kuboresha kituo cha mabasi Manyinga, ujenzi wa masoko maeneo ya Mlali, Madizini na Dakawa, uwezeshaji wa miche ya kokoa, karafuu, Michikichi na Parachichi kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara (TCCIA) Wilaya ya Mvomero Bw. Juma Sangai amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kudhibiti matukio ya kiharifu hususan wizi katika maeneo ya Madizini ambapo kwa sasa wafanyabiashara wanaendelea na biashara zao hata nyakati za usiku.
Baraza la Biashara la Wilaya linaundwa na Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti, Wajumbe 40 kutoka Sekta za Umma na Binafsi, Wajumbe 10 wa Kamati tendaji pamoja na Kamati kazi ya baraza hilo la Wilaya.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.