Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewaonya watumishi Wilayani humo juu ya matumizi mabaya ya mali za umma katika maeneo yao ya kazi kwani kwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Nguli ametoa onyo hilo Septemba 18, 2024 wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa ukusanyaji taarifa na mapato kielektroniki yaani GoTHoMIS katika vituo vya afya na Zahanati zilizopo katika Wilaya hiyo, mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mkuu huyo wa Wilaya amewataka kuacha kutumia mali ya Umma kwa maslahi yao binafsi badala yake watumie mali hizo kama ilivyoelekezwa na Serikali na kwamba atakae bainika kukiuka atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma ikiwemo kufukuzwa kazi, kushushwa cheo au kupunguzwa mshahara.
"...kitu kinachoitwa mali ya umma usikichezee..." amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Nguli ametoa kauli hiyo baada ya kukamatwa kwa dereva wa gari la kubeba wagonjwa (Ambulance) la Kituo cha Afya Chazi kilichopo Wilayani humo kwa kosa la kubeba abiria kinyume na miongozo ya Wizara ya Afya huku akibainisha kuwa tayari dereva huyo amechukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia mfumo huo wa GoTHoMIS, Mkuu huyo wa Wilaya amesema mfumo utasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato, upatikanaji wa takwimu za wagonjwa ambazo zitasaidia katika mipango ya uboreshaji wa Sekta ya Afya. Aidha, amewataka kwenda kufanyia kazi mfumo huo ili kuleta matokeo chanya katika Wilaya hiyo.
Awali wakati akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Philipina Philipo amesema mfumo huo unarahisisha ufuatiliaji wa utoaji huduma za Afya, kujua idadi ya wagonjwa waliopata huduma na kiasi cha mapato yaliyokusanywa katika Zahanati au Kituo cha Afya husika.
Ameongeza kuwa mfumo wa GoTHoMIS uliokuwa ukitumika awali ulikuwa na mapungufu ikiwemo kupelekea kupotea kwa mapato ambao katika Wilaya hiyo Vituo 13 vilifungwa mfumo huo lakini kwa sasa ni Vituo vya Afya vyote na Zahanati vitafungwa mfumo huo mpya ambao ni rahisi kutumia.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.