Kufuatia kifo cha Diwani wa Kata ya Mtibwa Mhe. Majaliwa Kayanda kilichotokea Agosti 26, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ametoa maelekezo kwa Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Watendaji wa Vijiji kuhakikisha kuwa wanaisimamia kwa karibu kata hiyo kama ambavyo diwani huyo alivyokuwa akiwajibika wakati wa uhai wake.
Mhe. Nguli ametoa maelekezo hayo Agosti 27, 2024 wakati akitoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali kwenye mazishi ya Diwani wa Kata hiyo ya Mtibwa yaliyofanyika katika Kata hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kifo cha Diwani huyo ni pengo hususan katika utendaji huku akitokea maelekezo kwa Wenyetivi wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji kusikiliza wananchi na kutatua kero zao wakati Serikali ikifanya utaratibu wa kuziba pengo hilo.
“…nitoe maelekezo kwao kuendelea kuingalia Kata kwa macho ya karibu sana kama ambavyo Mhe. Diwani alikuwa akiiangalia…” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mhe. Nguli amebainisha kuwa mafanikio ya Halmashauri hiyo ni kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Wahe. Madiwani akiwemo diwani wa Kata hiyo ya Mtibwa huku akisema kuwa Mhe. Majaliwa Kayanda amekuwa akipigania kuhakikisha anatatua changamoto za wananchi wa Kata hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mvomero Mhe. Yusuf Makunja ameiasa jamii kupendana hususan kipindi ambacho watu wote wapo hai.
Mhe. Majaliwa amezikwa katika makaburi ya familia yaliyopo katika Kata hiyo ya Mtibwa. Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.