Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amesema ataendelea kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanao kwepa kulipa kodi hii ni kutokana na kutofuata taratibu wakati wa kununua mazao kutoka kwa wakulima ikiwemo matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mhe. Nguli ametoa kauli hiyo Agosti 27, 2024 wakati akizindua Mnada wa kwanza wa Mbaazi kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani uliofanyika kwenye ghala lililopo katika Kata ya Sungaji, Kijiji cha Mbogo.
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa Halmashauri hiyo kupitia Baraza la Madiwani liliazimia mazao ya Ufuta, Alizeti, Mbaazi na Korosho yauzwe kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani lengo ni kuwainua wakulima ambao wanatumia gharama kubwa kwenye kilimo wakitarajia kupata faida.
“...na mimi nitaendelea kuyakamata magari yanayo torosha mbaazi, tena nitayakamata pasipo huruma...” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha, amesema Serikali inatekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 34 ambapo imeelekeza mazao yote ya kimkakati yaingizwe kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ili kumuinua mkulima.
Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Sungaji Bw. Clemence Kakuo amesema mfumo huo unalenga kuwaondoa walanguzi ambao wamekuwa wakinufaika kwa kununua mazao ya wakulima kwa shillingi 30,000 kwa debe huku wao wakiuza kwa bei ya juu hivyo amesema kupitia mnada huo mkulima anatarajia kupata shillingi 40,000 kwa debe.
Ameongeza kuwa hadi kufikia Agosti 27, 2024 jumla ya tani 95 ambazo zinatarajiwa kuuzwa kwa njia ya kielektroniki ambapo wanunuzi na bei ya mazao yatafanyika kwa njia ya mtandao.
MWISHO.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.