DC Mvomero ahamasisha Boda boda, Mama lishe kujiandikisha Daftari la Mkaazi.
Ikiwa zoezi la kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga wa Serikali za Mitaa likielekea ukingoni, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli ameendelea na juhudi za kuhamasisha makundi mbalimbali ya wananchi Wilayani humo yakiwemo waendesha boda boda, maguta na mama lishe kujiandikisha katika daftari hilo ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Mhe. Nguli ametoa rai hiyo kwa makundi hayo Oktoba 19, 2024 kwenye mkutano wa kuhamasisha wananchi kujiandikisha uliofanyika katika Kitongoji cha Mji Mwema huku akisisitiza umuhimu wa kujiandikisha mapema ili kuhakikisha wanatumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaostahili.
Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa kujiandikisha kwenye Daftari la wapiga Kura wa Serikali za Mitaa ni hatua muhimu kwa waendesha boda boda, kwani inawapa nafasi ya kushiriki kwenye maamuzi ya kitaifa yanayoweza kuleta mabadiliko katika sekta ya usafiri na huduma za jamii. Amesema kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuchagua viongozi watakaosaidia kuboresha mazingira yao ya kazi na kuleta maendeleo.
Kwa upande wa mama lishe, Mhe. Judith Nguli amewahimiza kujitokeza na kujiandikisha ili kuwa sehemu ya mchakato wa uchaguzi na kuhakikisha sauti zao zinasikika. Pia amebainisha kuwa kuchagua viongozi bora kunaweza kuleta fursa zaidi za kiuchumi kwa wanawake wajasiriamali, ikiwa ni pamoja na mikopo na mafunzo ya ujasiriamali.
Sambamba na hayo Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa makundi yote kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanajiandikisha na kutumia haki yao ya kupiga kura huku akiongeza kuwa ushiriki wao utasaidia kuimarisha demokrasia na kuchochea maendeleo endelevu katika wilaya ya Mvomero na nchini kwa ujumla.
Kwa upande wake Bw. Thomas John kwa niaba ya waendesha boda boda wengine amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya na kuahidi kuwa watahakikisha kuwa wanahamasishana ili waweze kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kuchagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa.
Pamoja na mkutano huo, Mkuu wa Wilaya alianza kutoa hamasa hiyo ya kujiandikisha katika vitongoji vya KKKT, Kitolondo na Mnazi Mmoja.
"Serikali za Mitaa, Sauti za Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi".
MWISHO
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.