Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Maulid Dotto, amewapongeza Wakuu wa Taasisi, Idara na Vitengo kwa juhudi kubwa wanazozionesha katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hali iliyosaidia kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi wilayani humo.
Akizungumza Julai 14, 2025 katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi hao, Mhe. Dotto amesema kazi nzuri inayoendelea kufanywa na watendaji hao ni ishara ya kujituma na kuipenda kazi, huku akisisitiza kuwa kuna haja ya kuongeza kasi ya uwajibikaji ili kuyafikia malengo ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
“...niwapongezeni kwa utekelezaji wa majukumu yenu yaliyowezesha kuleta matokeo chanya katika utendaji wa kazi zenu wito wangu kwenue mtupe ushirikiano ili tuweze kuyakamilisha yale ambayo yameachwa na watangulizi wetu..." amesema Mhe. Dotto.
Aidha, amewataka viongozi hao kuhakikisha matumizi ya rasilimali za umma yanazingatia uadilifu na thamani halisi ya fedha, huku akiweka wazi kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa kwa viongozi wa ngazi zote katika kufanikisha ajenda ya maendeleo jumuishi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Ndg. Paulo Faty akitoa taarifa ya maendeleo ya Halmashauri hiyo amesema kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia fedha kutoka Serikali kuu pamoja na mapato ya ndani huku akibainisha kuwa inaendelea kusimamiwa ili iweze kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.
Kwa upande wao baadhi ya watendaji waliopata fursa ya kutoa maoni yao akiwemo Bw. Karim Kanyamala amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akisema kuwa maelekezo aliyoyatoa watayafanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Wami Sokoine, Dakawa, Mvomero
Anwani Ya Posta: P.O BOX 663, MOROGORO
Msaada wa Kiufundi: +255 23 293 4348
Mobile: +255 23 293 4348
Baruapepe: ded@mvomerodc.go.tz
Hakimiliki ©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.Haki zote zimehifadhiwa.